DR Congo yakanusha kuingia makubaliano ya kijeshi na Urusi
Nairobi – Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekanusha ripoti kwamba imetia saini mkataba wa ushirikiano wa kijeshi na Urusi.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Katika taarifa ya wizara ya mawasiliano na vyombo vya habari nchini DR Congo siku ya Alhamisi, hakuna makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi yaliyotiwa saini hivi karibuni kati ya Urusi na Kinshasa .
#RDC Aucun accord de coopération militaire n’a été signé récemment entre la Russie et la République Démocratique du Congo 🇨🇩 - Mise au point ⤵️ pic.twitter.com/tFSt09dFk6
— Ministère de la Communication et Médias/RDC (@Com_mediasRDC) March 7, 2024
Taarifa hiyo ya serikali imekuja baada ya ile iliyochapishwa na shirika la habari la serikali ya Urusi TASS siku ya Jumanne, ambayo ilisema kuwa serikali ya Urusi iliidhinisha rasimu ya makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi na DR Congo.
Kwa mujibu wa TASS makubaliano hayo yalihusisha mazoezi ya pamoja, mafunzo ya kijeshi na masuala mengine ya kiusalama.
DR Congo inasema rasimu ya makubaliano husika ilianzishwa na nchi hizo mbili mwaka 1999, lakini bado haijatiwa saini.
Urusi imekuwa ikikuza mikataba yake ya kijeshi na nchi za Kiafrika huku ikijaribu kupanua ushawishi wake wa kisiasa katika bara hilo.
Kupitia kundi la mamluki la Wagner, Urusi imekuwa ikitoa msaada wa kijeshi kwa Jamhuri ya Afrika ya Kati na serikali zinazoongozwa na serikali za Mali, Niger na Burkina Faso.