Pata taarifa kuu

Madaktari nchini Kenya wasitisha mgomo wa kitaifa baada ya siku 56

Chama cha Madaktari nchini Kenya kimetangaza kusitisha mgomo wa kitaifa ulioanza mwezi Machi, baada ya kutia saini mkataba na serikali Jumatano jioni jijini Nairobi baada ya mazungumzo ya siku kadhaa.

Davji Attelah Katibu Mkuu wa chama cha Madaktari nchini Kenya, akitia saini mkataba wa kusitisha mgomo, Mei 08 2024 Davji Attelah Katibu Mkuu wa chama cha Madaktari nchini Kenya, akitia saini mkataba
Davji Attelah Katibu Mkuu wa chama cha Madaktari nchini Kenya, akitia saini mkataba wa kusitisha mgomo, Mei 08 2024 © MOH_Kenya
Matangazo ya kibiashara

Hata hivyo, undani wa mkataba huo haujawekwa wazi lakini uongozi wa Madaktari umesema kuwa, umeafikia maamuzi hayo baada ya mashauriano ya muda mrefu katika Kamati kuu ya chama chao.

Madkatari hao walitaka nyongeza ya mshahara, kuboreshewa mazingira ya kufanya kazi na kulipwa kwa Madaktari wanafunzi kwa mujibu wa mkataba waliokuwa wamekubaliana na serikali iliyopita mwaka 2017, Shilingi za nchi hiyo 206,000.

Davji Attelah Katibu Mkuu wa chama cha Madaktari nchini humo amesema, baada ya mashauriano ya muda mrefu, wamekubali kutia saini mkataba wa kusitisha mgomo.

“Mgomo ulioanza Machi 13 2024 umefika mwisho. Madaktari watafika kazini ndani ya saa 24 zijazo,” alisema Attelah.

Kuhusu suala tata la Madaktari wanafunzi kulipwa mshahara waliotaka, muungano huo umesema mwafaka haujapatikana, lakini imekubaliwa kuwa mashaurinao zaidi yaendelee.

Naye Waziri wa afya, Susan Nakhumicha, amesema serikali imeridhika kuwa mgomo huo umefika mwisho.

“Nawashukuru Madaktari kwa kukubali kusitisha mgomo. Wagonjwa sasa wataendelea kutibiwa,” alisema.

Tangazo la kusitishwa kwa mgomo ni habari njema kwa wagonjwa ambao wamekuwa wakiteseka wanapokwenda kwenye hospitali za umma kupata huduma za afya.

Baada ya hatua hii, Wakenya wanasubiri kuona namna mkataba huo utakavyotekelezwa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.