DRC: Mapigano yaripotiwa kati ya FARDC na M23 Kilolirwe na Kitshanga
Nairobi – Mapigano yalizuka tena hapo jana kati ya jeshi la Serikali ya DRC, FARDC na M23 kwenye maeneo ya Kilolirwe na Kitshanga, wilayani masisi jimboni Kivu Kaskazini, baada ya siku chache za kusitisha mapigano.
Imechapishwa:
Cheza - 00:44
Hali imeripotiwa kuwa ya wasiwasi katika mji wa Kishanga, ambako vyanzo kadhaa vimedai kuwa wanajeshi wa Burundi waliondoka kwenye eneo hilo baada ya kambi yake kushambuliwa, taarifa ambazo hata hivyo bado hazijathibitishwa na jeshi la kikanda la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aidha hali ya utulivu iliripotiwa kwenye mji wa Rutshuru, baada ya mapigano makali yaliyohusisha silaha nzito siku ya Jumanne.
Mashirika ya kiraia kwenye maeneo hayo, yameripoti vifo vya watu na wengine mamia kujeruhiwa, ingawa mamlaka hazijatoa takwimu rasmi kuhusu watu waliopoteza maisha katika mapigano hayo.
Mapigano haya yameripotiwa ikiwa ni siku mbili tangu kikosi cha umoja wa Mataifa, MONUSCO kutangaza operesheni za pamoja na jeshi la Serikali inayofahamika kama Springbok, dhidi ya waasi hao na makundi mengine.