Kenya: Polisi wanakabiliana na waandamanaji katika maeneo tofauti
Nairobi – Waandamanaji wa upinzani nchini Kenya wameendelea na maandamano yaliyopangwa siku ya Jumatano, kukaidi onyo kutoka kwa polisi walioyataja maandamano hayo kuwa haramu.
Imechapishwa:
Polisi wametumia vitoa machozi kuwatawanya waandamanaji katika miji mbalimbali huku mkuu wa polisi akisema ni sharti hatua muhimu zichukuliwe ili kuwatawanya.
Waandalizi wa maandamano wanatoa wito wa kufutwa kwa sheria mpya ambayo inaongeza maradufu ushuru wa mafuta na kuweka ushuru wa nyumba wa 1.5% kwa wafanyikazi. Kwa sasa imesitishwa na mahakama kuu jijini Nairobi, kwa sababu ya masuala ya kikatiba.
Lakini serikali inasema hatua hiyo ni muhimu kurekebisha masuala ya ulipaji wa deni na kuunda nafasi za kazi kwa vijana wasio na ajira.
Ijumaa iliyopita, makabiliano kati ya waandamanaji wa upinzani na polisi yalisababisha vifo vya watu sita katika miji mingi.
Siku ya Jumatano, barabara kuu katika jiji kuu la Nairobi pamoja na Kisii, Kisumu na Nyeri hazina shughuli nyingi, na video za mtandaoni zinaonyesha barabara zilizofungwa katika maeneo kadhaa. Madereva wa mabasi na teksi wamejiunga na maandamano hayo, wakielezea wasiwasi wao kuhusu kupanda kwa gharama ya mafuta.
#MaandamanoWednesday: Matatu operators in Nyeri halt operations as strike takes effect pic.twitter.com/uu0kVgSRrJ
— Radio Citizen (@RadioCitizenFM) July 12, 2023
Mtu mmoja ameripotiwa kufariki katika maandamano ya leo baada ya kupigwa risasi kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo. Baadhi ya miundo mbinu ikiwemo barabara zimeharibiwa.
Protesters bring down the Nairobi Expressway fence at Mlolongo #MaandamanoWednesday pic.twitter.com/4sE18vmeDW
— Radio Citizen (@RadioCitizenFM) July 12, 2023
Kando na hayo, picha zilizosambazwa mitandaoni zimeonyesha gari la polisi likiwa limechomwa moto katika maandamano ya leo. Biashara nyingi zimesalia kufungwa, na usafiri umesimama.