Pata taarifa kuu

Kenya: Rais Ruto ameidhinisha muswada wa fedha 2023 kuwa sheria

Nairobi – Rais wa Kenya William Ruto ametia saini kuwa sheria mswada wa kuongeza ushuru kwa bidhaa mbalimbali, na kukaidi ukosoaji kwamba hatua hiyo itawaongezea matatizo zaidi ya kiuchumi kwa wananchi wa taifa hilo.

Rais wa Kenya William Ruto ametia saini muswada wa fedha 2023 kuwa sheria
Rais wa Kenya William Ruto ametia saini muswada wa fedha 2023 kuwa sheria © Statehouse Kenya
Matangazo ya kibiashara

Mpango huo mpya wa ushuru uliidhinishwa na bunge wiki jana na utaongeza ushuru maradufu hadi asilimia 16 na kuanzisha kwa makato yanayolenga kuekelezwa kwa mradi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu, hatua inayotarajiwa kuwa na athari za kiuchumi kwa taifa hilo linalokabiliwa na mfumuko wa bei za bidhaa.

"Rais Ruto ameidhinisha mswada wa fedha. Umetiwa saini katika Ikulu," afisi ya rais ilisema katika ujumbe kwa wanahabari, ikiandamana na picha zake akitia saini muswada huo.

Ruto ambaye aliingia madarakani Septemba baada ya uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali, analenga kujaza hazina ya serikali iliyopungua na kukarabati uchumi wenye madeni makubwa uliorithiwa kutoka kwa mtangulizi wake Uhuru Kenyatta, ambaye aliingia katika miradi mikubwa ya miundombinu.

Sheria hii mpya inatarajiwa kuongeza mapato ya nchi hadi kufikia dola bilioni 2.1 ambapo kodi ya bidhaa muhimu kama chakuma, miamala ya simu na huduma nyingine itaongezwa.

Rais Ruto anasema serikali yake inalenga kuwajengea raia wake makazi bora
Rais Ruto anasema serikali yake inalenga kuwajengea raia wake makazi bora AFP - AMAURY FALT-BROWN

Hata hivyo moja ya kodi iliyoibua mjadala ni ile ya makazi nafuu, ambapo wafanyakazi nchini humo watakuwa wakikatwa asilimi 1.5 ya mshahara kila mwezi, ambapo pia muajiri atalipa kiasi sawa.

Kodi nyingine mpya ni ile ya asilimia tano ya maudhui ya watu wenye ushawishi mtandaoni.

Upinzani unaoongozwa na mpinzani wa Ruto, Raila Odinga umetishia kufanya maandamano mapya kuhusiana na mpango huo wa ushuru ukisema utaathiri mapato ya raia wa taifa hilo ambayo tayari yamebanwa.

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga © Raila Odinga

Mapema mwaka huu, upinzani ulifanya maandamano kulalamikia hatua ya kupanda kwa gharama ya maisha, maandamano yaliosababisha makabiliano makali kati ya maofisa wa polisi na  waandamanaji katika maeneo tofauti nchini humo.

Mamia ya waandamanaji wengine walikamatwa mwezi huu wakati wa maandamano dhidi ya mapendekezo ya ushuru yaliokuwa kwenye muswada huo wa 2023 ambao sasa umekuwa sheria.

Polisi nchini Kenya walikabiliana na wafuasi wa Odinga katika maeneo tofauti ya taifa hilo wakati wa maandamano ya awali
Polisi nchini Kenya walikabiliana na wafuasi wa Odinga katika maeneo tofauti ya taifa hilo wakati wa maandamano ya awali REUTERS - JAMES KEYI

Wakenya tayari wanakabiliwa na hali mbaya kutokana na kupanda kwa bei ya mahitaji ya kimsingi, pamoja na kushuka kwa kasi kwa thamani ya sarafu ya nchi hiyo na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika miongo minne.

Kwa sasa Kenya inadaiwa karibu dola za Marekani bilioni 70 ambayo ni sawa na asilimia 67 ya pato ghafi la nchi hiyo, ambapo pia gharama za ulipaji wa madeni yake zimeongezeka kutokana na tahamani ya sarafu yake kushuka hadi kufikia shilingi 145 dhidi ya dola ya Marekani.

Aidha watu ambao wanapokea shilingi laki 5 za kenya ambayo ni sawa na dola elfu 3 na 600, watakatwa kodi ya asilimia 32.5, huku wale wanaopokea shilingi laki 8 watakatwa asilimia 35 kutoka asilimia 30 ya sasa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.