Kenya: Polisi waonekana katika barabara za Nairobi kudhibiti maandamano
NAIROBI – Nchini Kenya, idadi kubwa ya maofisa wa polisi wa kupambana na ghasia wametumwa katika maeneo tofauti ya jiji kuu la Nairobi wakati huu upinzani nchini humo ukiitisha maandamano ya nchi nzima kupinga kile wanachosema ni kupanda kwa bei za bidhaa pamoja na masula mengine yakiwemo yanayohusu tume ya uchaguzi IEBC.
Imechapishwa:
Licha ya hayo, hali ya kawaida imeshuhudiwa katikati mwa jiji kuu la Nairobi japokuwa maeneo mengi ya biashara yamesalia kufungwa baadhi wakihofiwa kuwa huenda biahsara zao zikaporwa wakati wa maandamano hayo.
Idadi kubwa ya maofisa wa polisi pia imeshuhudiwa katika majengo ya tume ya uchaguzi IEBC, na majengo mengine ya serikali yaliokatikati mwa jiji kuu ambayo upinzani katika taarifa yake ulisema utazuru kupeleka lalama zao kwa wahusika.
Katika barabara ya Ngong, nje na jiji kuu la Nairobi, basi la abiria limeripotiwa kuchomwa moto kwa mujibu wa picha zilizochapishwa na vyombo vya habari vya ndani, watu waliokuwa wanataka kuaandamana wakidaiwa kuhusika na tukio hilo.
Tangu saa kumi na mbili na nusu kwa saa za Afrika Mashariki, vizuizi vya polisi vilionekana kuekewa katika barabara inayoelekea katika ofisi za Ikulu, huku maafisa wa polisi wakionekana katika barabara zinazoelekea kwenye Ikulu ya Nairobi.
Kando na Nairobi, maeneo mengine kama vile kaunti ya Kisumu, waandamanaji wameonekana wakiwa barabara kuitikia wito wa kiongozi wao, matairi ya magari yakiwa yamewashwa barabarani.
Maandamano ya leo Jumanne yanakuja wakati huu mkuu wa polisi jijini Nairobi Adamson Bungeiakiwa ameyaharamisha kwa msingi kuwa maandamano ya awali yaligeuka kuwa vurugu.
Licha ya polisi kukataa kutoa kibali cha kufanyika kwa maandamano hayo ya upinzani, Kinara wa Azimio la Umoja, Raila Odinga amesisitiza kuwa yatafanyika kama ilivyopangwa.