Kenya: Huenda mazungumzo kati ya upinzani na serikali yakagonga mwamba
NAIROBI – Nchini Kenya, ni wazi sasa huenda mazungumzo kati ya upinzani na Serikali yakagonga mwamba, baada ya kauli za hapo jana za rais William Ruto na kinara wa Azimio, Raila Odinga.
Imechapishwa:
Ruto sasa anamtaka kiongozi huyo kukubaliana na mchakato wa kibunge kupata suluhu au vinginevyo asubiri uchaguzi wa mwaka 2027.
"Nyinyi kama viongozi twendeni kule bunge tukaongee maneno ya viongozi kupitia bunge. Hakuna haja ya kuharibu biashara ya mwanachi."amesisitiza rais William Ruto.Rais wa Kenya William Ruto kuhusu Mazungumzo
Ni kauli ambayo hata hivyo haikupokelewa vizuri na Odinga, ambaye anasisitiza mchakato wa kibunge lazima uwe kwanza nje ya bunge, akitishia kuitisha tena maandamano ikiwa Serikali itashikilia msimamo wake.
"Tunasukumwa na wasiwasi kwamba licha ya katiba ya mwaka wa 2010, utamaduni wetu wa kisiasa unabaki kuwa mshindi ana mamlaka ya kila kitu, hii ndiyo imejitokeza wazi katika utawala uliopita."ameeleza Raila Odinga, kinara wa upinzani nchini Kenya.Raila Odinga, Kinara wa upinzani nchini Kenya kuhusu mazungumzo
Haya yanajiri baada ya juma lililopita, Odinga kutangaza kusitisha maandamano ya Jumatatu na Alhamisi, kuitikia wito wa rais Ruto kuhusu mazungumzo ya kupata suluhu.
Wito umekuwa ukitolewa kwa viongozi hawa wawili wa kisiasa kuketi pamoja na kutafuta suluhu la mvutano kama njia moja ya kuepusha taifa hilo kuingia katika machafuko ya kisiasa.
Suala la misimamo mikali kati ya mrengo wa Odinga na upande wa serikali ya rais Ruto likiajwa kuwa kizingiti kikubwa kwa kukwamisha mazungumzo.