Pata taarifa kuu
MAPINDUZI-DEMOKRASIA

Ufaransa yasitisha ushirikiano wa kijeshi na utawala mpya nchini Gabon

Waziri wa Majeshi ya Ufaransa Sebastien Lecornu anasema kuwa Paris imesitisha ushirikiano wa kijeshi na utawala mpya nchini Gabon. Haya yanajiri huku kiongozi Jenerali Brice Oligui Nguema akiapa kuwa taasisi za nchi zitakuwa za kidemokrasia zaidi, siku mbili baada ya kuongoza mapinduzi yaliyomaliza miaka 55 ya utawala wa familia ya Bongo.

Raia wakiwa na bendera ya taifa la Gabon wakisheherekea mapinduzi huko Libreville mnamo Agosti 30, 2023 baada ya kundi la maafisa wa kijeshi wa Gabon kuonekana kwenye televisheni wakitangaza "kuangusha utawala wa sasa".
Raia wakiwa na bendera ya taifa la Gabon wakisheherekea mapinduzi huko Libreville mnamo Agosti 30, 2023 baada ya kundi la maafisa wa kijeshi wa Gabon kuonekana kwenye televisheni wakitangaza "kuangusha utawala wa sasa". AFP - -
Matangazo ya kibiashara

Ufaransa ina takriban wanajeshi 400 nchini Gabon wanaotoa mafunzo kwa jeshi la nchi hiyo.

"Kwa sasa, shughuli zao zimesitishwa huku wakisubiri ufafanuzi wa hali ya kisiasa," Lecornu amenukuliwa akisema katika makala yaliyochapishwa kwenye gazeti la Le Figaro mtandaoni siku ya Ijumaa jioni.

Nchi nyingine tano barani Afrika - Mali, Guinea, Sudan, Burkina Faso na Niger - zimepitia mapinduzi katika miaka mitatu iliyopita. Watawala wao wapya wamepinga matakwa ya kupewa ratiba fupi ya kurejea kambini.

Ufaransa ililaani mapinduzi ya Jumatano nchini Gabon na imesisitiza nia yake ya kuona matokeo ya uchaguzi yanaheshimiwa ikirejelea kura za urais zenye utata za Jumamosi ya wiki iliyopita katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Siku ya Jumatano Jenerali Brice Oligui Nguema, mkuu wa kikosi cha walinzi wa Jamhuri, alimuondoa mamlakani rais Ali Bongo Ondimba.

Kuondolewa huko kulikuja muda mfupi tu baada ya Bongo, 64, kutangazwa mshindi wa uchaguzi- matokeo yaliyotajwa na upinzani kuwa ni udanganyifu mtupu.

Viongozi hao wa mapinduzi walisema wamevunja taasisi za taifa, kufuta matokeo ya uchaguzi na kufunga mipaka.

Oligui anatarajiwa Jumatatu kuapishwa kama "rais wa mpito".

Mipango ya kurejesha utawala wa kiraia

Lakini nchi nyingi hazijamtambua Jenerali Oligui kama kiongozi halali wa Gabon na anakabiliwa na shinikizo la kueleza mipango yake ya kurejesha utawala wa kiraia.

"Kuvunjwa kwa taasisi" hatua iliyotangazwa siku ya Jumatano wakati wa mapinduzi "ni ya muda," Oligui alisema katika hotuba. "Ni juu ya kupanga upya ili kuzifanya kuwa za kidemokrasia zaidi."

(Pamoja na AFP)

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.