Pata taarifa kuu

UN: Vita nchini Sudan vimesabababisha watu 700,000 kuyahama makwao

NAIROBI – Umoja wa Mataifa umesema kuwa mapigano makali nchini Sudan, yamesababisha zaidi ya watu laki saba kuyahama makazi yao. 

Watu wa Sudan wakiwa katika kambi ya wakimbizi katika Kaunti ya Renk, Sudan Kusini, Mei 3, 2023.
Watu wa Sudan wakiwa katika kambi ya wakimbizi katika Kaunti ya Renk, Sudan Kusini, Mei 3, 2023. © AP - Peter Louis
Matangazo ya kibiashara

Nchi ya Sudan imekuwa ikishuhudia mapigano tangu Aprili 15, baada ya mkuu wa jeshi Abdel Fattah Al-Burhan na naibu wake Mohammed Hamdan Daglo kutofautiana, mapigano ambayo yamesababisha maafa ya takriban watu 750.

Akizungumza na waandishi wa habari huko Geneva, msemaji wa shirika la kimataifa la uhamiaji IOM, Paul Dillon, amesema idadi ya watu waliokimbia makazi yao imeongezeka mara dufu tangu wiki iliyopita.

Wiki iliyopita, idai ya watu waliorekodiwa kuyahama makazi yao ilikuwa 340,000.

Dillon ameongeza kuwa hata kabla ya mapigano, raia milioni 3.7 walikuwa wamesajiliwa kama wakimbizi wa ndani kwa ndani.

Kutokana na mapigano haya, wale walioachwa nyuma katika maeneo ya vita wanakabiliwa na uhaba wa maji, umeme, chakula na huduma za matibabu katika nchi ambayo, kulingana na Umoja wa Mataifa, karibu theluthi moja ya watu wanahitaji msaada wa kibinadamu hata kabla ya mapigano kuanza.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa Jumatatu na shirika la wakimbizi UNHCR, watu wengine laki moja na elfu hamsini wamekimbia nchi hiyo tangu kuanza kwa vita ambavyo vimeendelea zaidi katika mji mkuu Khartoum, lakini maeneo mengine haswa eneo la Darfur magharibi linalopakana na Chad, pia yameshuhudia mapigano makali.

Kufikia sasa mazungumzo ya kuleta mapatano hayajafanikiwa, lakini baadhi ya nchi wamefanikiwa kuwahamisha raia wao kutoka nchi hiyo kupitia nchi kavu, baharini na angani.

Wakati huu mapigano haya yakiendelea kati ya majenerali hawa wawili, wasiwasi mpya umeibuka kufuatia mapigano tofauti ya kikabila ambayo yamegharimu maisha ya watu 16 katika eneo la kusini mwa nchi hiyo.

Umoja wa Mataifa umeelezea hali ya kibinadamu ya Sudan kuwa janga.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.