Pata taarifa kuu

Chad: WFP yakabiliwa na uhaba wa pesa za kulisha wakimbizi na watu waliokimbia makazi yao

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP linahitaji dola milioni 142.7 katika kipindi cha miezi sita ijayo ili kuendelea kupeleka chakula kwa wakimbizi na watu waliokimbia makazi yao nchini Chad.

Raia wa Cameroon waliokimbia machafuko ya kikabila kati ya wafugaji na wakulima wako katika kambi ya wakimbizi ya muda katika wilaya ya Farcha, Ndjamena, Chad, tarehe 9 Desemba 2021.
Raia wa Cameroon waliokimbia machafuko ya kikabila kati ya wafugaji na wakulima wako katika kambi ya wakimbizi ya muda katika wilaya ya Farcha, Ndjamena, Chad, tarehe 9 Desemba 2021. © REUTERS - MAHAMAT RAMADANE
Matangazo ya kibiashara

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) linaweza kusitisha msaada wake kwa mamia ya maelfu ya wakimbizi na watu waliokimbia makazi yao nchini Chad kuanzia mwezi Mei ikiwa halitapokea haraka fedha za ziada kutoka kwa nchi wafadhili, afisa mmoja ameonya leo Ijumaa.

"Hatuna tena msaada wa kifedha kuanzia mwezi Mei na kuendelea," ameelezea Pierre Honnorat, mkurugenzi wa WFP nchini Chad, wakati wa mkutano wa kawaida wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva.

WFP ina uhaba wa fedha kiasi kwamba mwezi Aprili ililazimika kupunguza idadi ya wakimbizi ambayo ina uwezo wa kusaidia kutoka 455,600 hadi 270,000 pekee.

Shirika hilo linahitaji dola milioni 142.7 kwa muda wa miezi sita ijayo ikiwa linataka kuendelea kutekeleza azma yake na kupeleka chakula kwa wakimbizi na watu waliokimbia makazi yao lakini pia kwa wananchi wengine wa Chad ambao wamekumbwa na hali mbaya ya hewa katika miaka ya hivi karibuni.

"Ikiwa hakuna ufadhili wa ziada, msaada wa chakula utakatwa kwa 100% mwezi Mei 2023 kwa wakimbizi na watu waliokimbia makazi yao," taarifa imesema.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi UNHCR limekadiria mahitaji yake kwa 2023 kuwa dola 172.5 milioni kwa Chad, kulingana na Matt Saltmarsh, msemaji wa UNHCR.

UNHCR hadi sasa imepokea tu 15% ya jumla ya kiasi hicho, ameongeza.

Maelfu ya watu, hasa wanawake, watoto na wazee, wamekimbia ghasia nchini Sudan katika wiki za hivi karibuni na kukimbilia Chad, na kuongeza changamoto ya usambazaji nchini humo.

Kulingana na takwimu zilizotolewa Ijumaa na WFP, Chad ina wakimbizi 583,400 waliosajiliwa na wakimbizi wa ndani 381,000.

Lakini uhaba wa chakula unaenea zaidi ya hapo na uliathiri watu milioni 1.9 mwezi Machi.

Baadhi ya watoto milioni 1.36 wanakabiliwa na utapiamlo mkali ambao husababisha kupungua kwa uzito wa wastani na hauhitaji kulazwa hospitalini.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.