Ukraine: Idadi ya waliofariki imeongezeka hadi 28, huduma za dharura za Urusi zasema
Idadi ya watu waliofariki kutokana na shambulio la siku ya Jumamosi, Februari 3 lililohusishwa na Ukraine kwenye duka la kuoka mikate katika jiji linalokaliwa la Lyssychansk (mashariki mwa nchi hiyo) imeongezeka hadi 28, akiwemo mtoto mmoja, idara ya huduma za dharura ya Urusi imetangaza siku ya Jumapili Februari 4.
Imechapishwa:
"Shughuli za utafutaji zinaendelea kwenye eneo la tukio, ambapo duka la kuoka mikate lilianguka (...) Takriban 65% ya muundo ulioharibiwa umevunjwa (...) Kwa bahati mbaya, watu 28, ikiwa ni pamoja na mtoto mmoja , walifariki," Wizara ya Hali za Dharura ya Urusi imesema kwenye Telegram, kulingana na shirika la habari la AFP.
Leonid Pasechnik, gavana wa Lugansk aliyewekwa rasmi na Urusi, anashutumu vikosi vya Kiev kwa kulenga duka kubwa la kuoka mikate ambalo anasema linajulikana kwa kuwa na mkate mzuri wakati wa wikendi.
Kwenye Telegram, Leonid Pasechnik, gavana wa Lugansk ametangaza siku moja ya maombolezo katika eneo hili lililokaliwa na jeshi la Urusi siku ya Jumapili.
Eneo la Lysychansk, katika jimbo la Lugansk, lilianguka mikononi mwa vikosi vya Urusi katika msimu wa joto wa mwaka 2022 baada ya vita vikali.
"Huko Lysychansk, maafisa wa Wizara ya Hali ya Dharura ya Urusi walitoa miili 15 ya wahanga kutoka chini ya vifusi," wizara hiyo imesema kwenye Telegram.
Chanzo hicho kilichapisha video ya waokoaji wakifanya kazi gizani, wakiondoa mwili kutoka kwenye kifusi kabla ya kugundua mwanamke aliyejeruhiwa ambaye alibebwa kwenye machela.
Wizara hiyo ilisema hapo awali kwamba imepanga kuendeleza zoezi la kutafuta manusura na miili ya watu iliyokwama chini ya vifusi "usiku kucha" na kwamba waokoaji hadi sasa "wameokoa watu 10" kutoka chini ya vifusi.
Jengo hilo la ghorofa moja lilikuwa na bango kubwa lenye jina la "Adriatic Restaurant" na lilionekana kuharibiwa kabisa.
Lysychansk, iliyoko kilomita 15 kutoka eneo linalodhibitiwa na Ukraine, lilikuwa na idadi ya wakazi 111,000 kabla ya mashambulizi ya Urusi kuanza.
(Pamoja na AFP)