Putin ameapishwa kuiongoza Urusi kwa muhula mwengine wa miaka sita
Raisi wa Urusi Vladimir Putin ameapishwa kuongoza nchi yake kwa kipindi kingine cha miaka sita baada yake kuibuka mshindi katika uchaguzi mkuu wa urais wa mwezi Machi mwaka huu.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Putin mwenye umri wa miaka 71, atawaongoza Warusi kwa muhula wake wa tano sasa.
Katika hotuba yake baada ya kuapishwa, Putin amewaeleza raia wa nchi yake kuwa wataibuka washindi baada ya kipindi kigumu.
Kiongozi huyo anatarajiwa kuiongoza nchi yake kwa mara nyengine tena baada ya kukabiliwa na masuala mabalimbali ikiwemo kuwanyamazisha wapinzani wake pamoja na kuivamia nchi jirani ya Ukraine katika kipindi cha muhula wake wa nne.
Putin kwa sasa ndiye rais ambaye ameiongoza nchi yake kwa kipindi kirefu zaidi tangu uongozi wake Josef Stalin, ambapo sasa ataongoza Urusi hadi mwaka wa 2030.
Katika hafla iliohudhuria na watu wachache mashuhuri, kiongozi huyo pia ameapa kuilinda nchi yake.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa Putin ameisaidia nchi yake pakubwa katika masuala ya kiuchumi tangu kuchukua uongozi kutoka kwa rais Boris Yeltsin mwaka wa 1999.
Tangu kuivamia nchi ya Ukraine mwaka wa 2022 katika vita ambavyo vimegeuka kuwa vikubwa zaidi barani Ulaya tangu vita vya pili vya dunia, Urusi imekabiliwa na vikwazo vikubwa kutoka kwa nchi za Magharibi.
Soma piaPutin kutawazwa kama rais wa Urusi kwa muhula wa tano
Kutokana na vikwazo hivyo, Urusi imeonekana kutafuta washirika wapya kutoka nchi za China, Iran na Korea kaskazini kwa uungwaji mkono na ushirika.