Pata taarifa kuu
USALAMA-ULINZI

Mashariki mwa DRC: Saba wauawa na kukatwa viungo vyao kaskazini mwa Goma

Takriban raia saba wameuawa na kukatwa viungo vyao  siku ya Jumanne karibu na Rumangabo, takriban kilomita 40 kaskazini mwa mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini, Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kulingana na shirika la habari la AFP likinukuu chifu wa eneo hilo na mashahidi.

Wakaazi wa eneo la Rumangabo wakihuzunishwa na visa vya mauaji vilivyokithiri.
Wakaazi wa eneo la Rumangabo wakihuzunishwa na visa vya mauaji vilivyokithiri. © REUTERS
Matangazo ya kibiashara

Wakati mapigano yakiongezeka katika siku za hivi karibuni kati ya jeshi la Kongo na wanamgambo wa ndani kwa upande mmoja na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda kwa upande mwingine kulingaana serikali ya DRC, watu saba wamepatikana wameuawa kwa kuchinjwa na kukatwa viungo vyao siku ya Jumanne asubuhi kwenye barabara ya kitaifa namba 2, katika eneo la Rutshuru.

Eneo hili lilirejeshwa rasmi na kundi la waasi wa M23 mwanzoni mwa mwaka kwa wanajeshi wa Kenya waliotumwa kama sehemu ya jeshi la Afrika Mashariki, linalopaswa kutoa ulinzi katika eneo lisilo kuwa na wanajeshi au wapiganaji kati ya pande hasimu. Waasi wa M23 walidumisha uwepo na udhibiti wa usafirishaji haramu wa watu na bidhaa kwenye sehemu za barabara ya kitaifa (RN 2) na katika vijiji vya karibu.

Usiku wa Jumatatu kuamkia Jumanne, watu "waliovalia sare za kijeshi na wengine waliovaa kiraia" waliwateka nyara watu saba kutoka kwa nyumba zao, akiwemo "chifu wa eneo la Bugoma (karibu kilomita 1 kutoka Rumangabo) na naibu wake", Patrick Ntamugabumwe, chifu wa eneo la Rumangabo, ameliambia shirika la habari la AFP. Kwa sharti la kutokutajwa jina, chanzo kingine kinaongeza kuwa wanajeshi kutoka jeshi la Afrika Mashariki walifika papo hapo siku ya Jumanne, "walifanya uchunguzi wao" kisha "wakaomba wahanga wazikwe".

Kulingana na mkazi aliyehojiwa kwa njia ya simu, "wengi wa waathiriwa ni viongozi wa kimila ambao walifanya kazi na M23." Kwenye X (zamani ikiitwa Twitter), 'kiongozi' wa kundi la M23, Bertrand Bisimwa, ameshtumu 'vikosi vya jeshi la DRC, FARDC na washirika wao kuwaua kikatili raia sita wasio kuwa na hatia".

Kwa upande wake, msemaji wa gavana wa kijeshi wa mkoa Kivu Kaskazini, Luteni Kanali Guillaume Ndjike, amewanyooshea kidole cha lawama "magaidi wa M23/RDF (Jeshi la Ulinzi la Rwanda, jina la jeshi la Rwanda)" akiwatuhumu kufanya "mauaji ya kinyama" dhidi ya raia wa DRC (...) kwa kisingizio kwamba jeshi la FARDC linashirikiana na Wazalendo (jina maarufu linalopewa makundi yenye silaha yanayopigana dhidi ya M23)".

Siku ya Jumatatu, shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu (OCHA) nchini DRC lilibaini kwamba takriban raia 20 wameuawa na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa tangu Oktoba 1 na "kuzuka tena kwa mapigano makali kati ya makundi yenye silaha" huko Kivu Kaskazini.

Waziri wa Mawasiliano na msemaji wa serikali, Patrick Muyaya, alitangaza wakati wa mkutano na waandishi wa habari Jumatatu jioni kwamba "anakaribisha hatua ya watu hawa", akimaanisha "vijana" wanaokabiliana na M23. "Ni wajibu wa kila Mkongo kutetea kila sentimita ya eneo la taifa," alisema, akibainisha kwamba jeshi la Kongo "linaheshimu makubaliano ya usitishaji mapigano."

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.