Pata taarifa kuu

Sudan: Mapigano yaendelea huku hali ya kibinadamu ikiibua wasiwasi

NAIROBI – Licha ya kuwepo kwa  makubaliano ya kusitisha vita kati ya jeshi la taifa na wapiganaji wa RSF, mapigano yameendelea kushuhudiwa kwa siku ya 20 leo jijini Khartoum.

Upande wa kushoto, mkuu wa vikosi vya jeshi la Sudan, jenerali al-Burhan na upande wa kulia mkuu wa Vikosi vya RSF, Jenerali Hemedti.
Upande wa kushoto, mkuu wa vikosi vya jeshi la Sudan, jenerali al-Burhan na upande wa kulia mkuu wa Vikosi vya RSF, Jenerali Hemedti. AFP - ASHRAF SHAZLY
Matangazo ya kibiashara

Kuanzia leo alfajiri, milio ya risasi na milipuko ya bomu imesikika karibu na makaazi ya rais na makao makuu ya Jeshi.

Mbali na Khartoum, makabiliano yameshuhudiwa katika miji ya Omdurman na Bahri.

Mapema Alhamisi, jeshi lilisema lilikuwa limekubali pendekezo la kusitisha mapigano kwa siku saba zaidi, na kutaka matatizo ya nchi yake kusuluhishwa na bara la Afrika.

Nalo kundi la RSF linadai kuwa linadhibiti asilimia 90 ya jiji la Khartoum, na kuongeza kuwa linafungua barabara ili kuruhusu kupita kwa misaada ya kibinadamu na watu wanaokimbia nchi hiyo.

Picha iliyopigwa Mei 4, 2023 huko Khartoum, mji mkuu wa Sudan. Milio ya risasi na milipuko ilitanda Khartoum kwa siku ya 20 mfululizo, na kuacha juhudi za hivi punde za kusitisha mapigano.
Picha iliyopigwa Mei 4, 2023 huko Khartoum, mji mkuu wa Sudan. Milio ya risasi na milipuko ilitanda Khartoum kwa siku ya 20 mfululizo, na kuacha juhudi za hivi punde za kusitisha mapigano. AFP - -

Kiongozi wa waasi wa Sudan aliye uhamishoni nchini Sudan Kusini, Abdel Wahid Nur, ambaye pia ni mzoefu wa miongo kadhaa ya mapigano katika eneo la Darfur, amesema kwamba hakuwezi kuwa na mshindi katika vita vinavyoendelea kati ya majenerali hasimu abdel Fatah al-Burhan na Mohamed Hamdan Daglo, akisema raia nchini Sudan wanataka serikali ya kiraia.

Umoja wa Mataifa unasema hali ya kibinadamu inaendelea kuwa mbaya, na inataka pande zinazopigana, kutoa hakikisho la usalama wa wafanyakazi na misafara iliyobeba misaada ya kibinadamu kama chakula na dawa.

Aidha, Umoja wa Mataifa unasema mpaka sasa watu Laki Moja wamekimbia nchi hiyo huku mamia wakiripotiwa kupoteza maisha.

Shirika la umoja wa mataifa linalowashughulikia wakimbizi, UNHCR limesema kwamba takriban dola milioni 445 zinahitajika ili kuwasaidia watu ambao wanakadiriwa huenda wakakimbia Sudan kufikia mwezi Oktoba, kutokana na mapigano yanayoendelea.

UNHCR sasa inatoa wito kwa nchi wafadhili kusaidia katika upatikanaji wa fedha hizo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.