Pata taarifa kuu
GAMBIA-SIASA-USALAMA

Mwasisi wa uhuru Gambia, Dawda Jawara afariki dunia

Rais wa kwanza wa Gambia na mwasisi wa uhuru wa nchi hiyo, Dawda Jawara, amefariki dunia Jumanne, Agosti 27 akiwa na umri wa miaka 95. Familia yake imethibitisha kifo chake na kusema kuwa kimetokea katika makazi yake huko Fajara, kilomita 15 kutoka mji mkuu Banjul.

Mwasisi wa uhuru na mwanzilishi wa Jamhuri ya Gambia, Dawda Jawara, amefariki dunia Agosti 27, 2019 akiwa na umri wa miaka 95.
Mwasisi wa uhuru na mwanzilishi wa Jamhuri ya Gambia, Dawda Jawara, amefariki dunia Agosti 27, 2019 akiwa na umri wa miaka 95. © Gambia Presidency/Handout via REUTERS
Matangazo ya kibiashara

Dawda Jawara alikuwa rais mkongwe zaidi wakati alitimuliwa madarakani mnamo mwezi Julai 1994. Wakati huo alikuwa ametumia zaidi ya miaka 24 akiwa mkuu wa Jamhuri ya Gambia.

Kabla ya hapo, Dawada Jawara, ambaye alizaliwa mnamo mwaka1924, alisomea nchini Scotland. Alirudi nchini mwake mwanzoni mwa miaka ya 1950 kama daktari wa mifugo na alianza kujishughulisha na siasa mwaka 1960 baada ya kujiunga na Chama cha Progressive People.

Mwanzilishi wa Jamhuri ya Gambia

Alihudumu kama waziri mkuu kwa miaka mitatu wakati Gambia ilipata uhuru kutoka kwa Uingereza mnamo mwaka 1965. Alianzisha Jamhuri ya Gambia miaka mitano baadaye na akawa rais wa kwanza wa nchi hiyo.

Alipata usaidizi kutoka Senegal dhidi ya jaribio la mapinduzi lililoendeshwa mnamo mwaka 1981 na akaanzisha ushirika wa kikanda uliojulikana kwa jina la Senegambia mnamo mwaka 1982 na rais wa Senegal Abdou Diouf.

Mapinduzi ya kijeshi ya 1994 yaliyoongozwa na Yahya Jammeh yalipindua serikali iliyochaguliwa kidemokrasia ya Dawda Jawara. Dawda Jawara aliamua kuondoka nchi hiyo na kwenda kuishi nchini Senegal. Alishangiliwa na kusamehewa aliporudi Gambia mnamo mwaka 2010.

"Nchi imepoteza mtu muhimu"

Rais wa Gambia Adama Barrow ameandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa Twitter, akibaini kwamba nchi ya Gambia imepoteza mtu muhimu, huku akitoa rambi rambi zake kwa familia ya Dawda Jawara na wananchi wa Gambia.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.