Pata taarifa kuu
DRC

Kagame na Museveni wakanusha kuwasaida waasi wa M 23 mbele ya UN

Marais wa Rwanda na Uganda wameueleza Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa unaotembelea eneo la Ukanda wa Maziwa Makuu wao hawajahusika kwa namna yoyote na ukosefu wa amani unaoshuhudia Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Matangazo ya kibiashara

Wajumbe kutoka Mataifa 15 wanachama wa Kudumu wa Baraza la Usalama walikutana na Rais wa Rwanda Paul Kagame na kisha Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda ambao wote wamekana kuhusika na tuhuma za wao kuwasaidia Waasi wa M 23 wanaolemaza hali ya usalama ya Mashariki mwa DRC.

Licha ya kauli hizo kutoka kwa Marais hao lakini wajumbe wa Baraza la Usalama wamesisitiza ni lazima washiriki katika kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana katika eneo hilo.

Umoja wa Mataifa unazituhumu Rwanda na Uganda kuwaungana mkono waasi wa M 23 wanaoendelea kupambana na jeshi la serikali ya Jamhuri ya Kidemokraia ya Congo tuhma ambazo Kampala na Kigali zinasema hazina msingi wowote.

Ziara ya wajumbe hao nchini Rwanda na Uganda inakuja baada ya Marekani wiki iliyopita kutangaza kuiwekea vikwazo serikali ya Kigali ikiwa ni pamoja na kusitisha mafunzo na ufadhili wa jeshi lake kwa kuendelea kuwaunga mkono waasi wa M 23 wanaotumia watoto katika jeshi lake.

Umoja wa Mataifa unasema utulivu Mashariki mwa DRC unaweza kupatikana tu kupitia mazungumzo ya kisiasa wala sio matumizi ya nguvu.

Aidha, Umoja wa Mataifa unasema mazungumzo ya amani yanayoendelea jijini Kampala ni muhimu sana na ni sharti yapewe nafasi ili suluhu lipatikane ili amani irejee Mashariki mwa DRC.

Mazungumzo hayo kati ya waasi wa M 23 na wajumbe wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yamekuwa yakiendelea kwa wiki kadhaa na hadi sasa hakuna muafaka wowote uliopatikana.

Mwezi uliopita, Marais wa Kanda ya Maziwa Makuu walikutana jijini Kampala na kuwapa wajumbe kutoka pande zote mbili wiki mbili kupata suluhu ambalo hadi sasa bado halijapatikana.

Hata hivyo, serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tayari imetoa orodha ya baadhi ya waasi wa M 23 watakaojumuishwa katika jeshi la serikali au kupewa msamaha ikiwa suluhu litapatiana.

Makabiliano kati ya waasi wa M 23 na jeshi la serikali yamesababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na wengine kukimbia makwao.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.