Pata taarifa kuu
Tenisi

Mchezo wa Tennis wapata viongozi wapya barani Afrika

Nairobi – Jiji la Nairobi nchini Kenya lilikua mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa shirikisho la tenisi barani Afrika, mkutano ambao pia ulikua mkutano wa uchaguzi na rais wa shirikisho la tenisi la kimataifa, David Haggerty alihudhuria.  

Mchezo wa Tennis
Mchezo wa Tennis AFP - GLYN KIRK
Matangazo ya kibiashara

Kwenye uchaguzi huo – Jean Claude Talon kutoka Benin alichaguliwa rais baada ya kupata kura 25 dhidi ya Nelson Amanze wa Botswana – 12, Issa Mboup wa Senegal-9.  

“Ninafurahi sana luwa wajumbe wameniamini kiasi hiki. Nitafanya kadri ya uwezo wangu kuboresha tenisi ya Afrika,” alisema Talon ambaye anaridhi mikoba ya rais anayeondoka Tarak Cherif ambaye muda wake ofisini ulikamilika. 

“Mpango wangu wa kwanza ni kupata uungwaji mkono na serikali zetu. Hili litatusaidia kujenga viwanja, kuandaa mashindano zaidi na watoto wengi watajiunga na tenisi na Afrika tutazalisha mchezaji bora duniani,” alikariri Talon. 

Kwenye kura za urais wa kanda za Afrika – katibu mkuu wa Tenisi nchini Kenya, Wanjiru Mbugua Karani alichaguliwa kuwa rais wa ukanda wa Afrika Mashariki na naibu rais wa Tenisi barani Afrika – hivyo kuweka historia kuwa mwanamke wa kwanza kuwa rais ukanda huu na wa pili kuchaguliwa naibu rais Afrika. 

“Nimefurahi sana kuwa rais wa kwanza mwanamke ukanda huu na wa pili barani Afrika,” Wanjiru alionyesha furaha yake akiwa na tabasamu kubwa usoni. 

 

Wanjiru Mbugua, alichaguliwa kuwa rais wa Shirikisho la mchezo wa Tennis Afrika Mashariki
Wanjiru Mbugua, alichaguliwa kuwa rais wa Shirikisho la mchezo wa Tennis Afrika Mashariki © Jairus Mola -Tennis Kenya Media

Je, mipango yako ni ipi kwa Afrika Mashariki unapoingia kwenye ofisi kuu?

Wanjiru Mbugua alisisitiza Afrika Mashariki ina talanta chungu nzima akitoa mifano ya Saada Nahimana wa Burundi na Angella Okutoyi wa Kenya ambaye amecheza katika ngazi za juu zaidi duniani. 

“Sasa ni kuhakikisha tunawapa wengine fursa ya kukua pia. Nina wazo la kuanzisha kambi ya mazoezi kwenye ukanda huu wakati wa kila likizo ambapo tutajifunza miongoni mwetu na kukuza tenisi pamoja,” alitilia mkazo Wanjiru Mbugua-Karani ambaye amejaza nafasi ya rais anayeondoka Dkt. Patrick Gichira. 

Wanjiru Mbugua alimshinda rais wa Tenisi nchini Comoros Mahamoud Zayya kwa kura 6-5 kwenye duru ya pili uchaguzi baada ya sare ya 5-5 kwenye awamu ya kwanza. 

Kwenye kanda zingine, Abdelaziz Laaraf kutoka Morocco alishinda urais wa Afrika Kaskazini, Ifedayo Akindoju kutoka Nigeria akishinda ukanda wa magharibi, Germain Ickonga kutoka Congo ataiwakilisha Afrika ya Kati naye Jonas Alberto akichaguliwa rais wa kusini mwa Afrika. 

Rais wa tenisi la kimataifa ITF, David Haggerty alikua miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo.  

Naye alisema, “mara nyingi ninapohudhuria mikutano mikuu hua nasikiliza mataifa husika ili kuelewa namna gani tutakabili changamoto katika harakati za kuboresha tenisi kwenye bara hilo. ” 

Hii ilikuwa ziara ya pili kwa David Haggerty nchini Kenya baada ya ziara yake nchini humo mwezi Mei mwaka 2017 alipoongoza katika ufunguzi wa chuo cha mafunzo cha tenisi jijini Nairobi. 

Haggerty amekua rais wa tenisi la kimataifa tangu mwaka 2015 katika uchaguzi wa kwanza na mnamo Septemba mwaka 2023, alichaguliwa tena kwa muhula mwingine wa miaka minne (utakaoisha mnamo 2027) kwa zaidi ya asilimia 70 ya kura za wajumbe katika Mkutano Mkuu wa ITF huko Cancun, Mexico. 

Bw. Haggerty pia ni mjumbe wa bodi katika Olimpiki ya Kimataifa. 

Rais wa Shirikisho ma mchezo wa Tennis nchini Kenya, Wanjiru Mbugua na mwenzake kutoka Tunisia, Salma Mouelhi
Rais wa Shirikisho ma mchezo wa Tennis nchini Kenya, Wanjiru Mbugua na mwenzake kutoka Tunisia, Salma Mouelhi © Jairus Mola - Tennis Kenya Media

Kujifunza kutoka kwa wenzako ndio njia ya kujiboresha 

Mataifa ya kaskazini mwa Afrika yanaongoza katika mchezo huu barani. Tunisia inashikilia nafasi ya kwanza barani Afrika katika msimamo wa dunia katika nafasi ya 52, Misri, Morocco na Afrika Kusini zinafuata katika nafasi za 55, 57, 58 mtawalia.

Kenya inaongoza katika ukanda wa Afrika Mashariki katika nafasi ya 98 ikifuatwa na Rwanda katika nafasi ya 100, Uganda ipo nafasi ya 140. 

Kwa upande wa kina dada, Misri inaongoza barani Afrika katika nafasi ya 47 ikifuatiwa na Afrika Kusini nafasi ya 57, Morocco -90, Tunisia -93, Uganda -114, Kenya -116, Rwanda -119.

Rais wa tenisi nchini Tunisia, Salma Mouelhi, anatathmini kuwa mchezo huu unaendelea kukua kila mwaka na “tuko na wachezaji wengi sana na mnajua mchezaji bora Afrika alikua nambari mbili kwa sasa yupo nambari saba duniani anatoka Tunisia. ” 

“Pia idadi ya wachezaji wa Afrika inaongezeka pakubwa na nadhani kwa miaka minne ijayo Afrika itatawala kwa asilimia kubwa duniani,” aliongezea Salma. 

Tunalenga wachezaji wetu kupanda katika nafasi za mia moja kuenda juu kwa chipukizi au wa kitaalamu.

Ons Jabeur kutoka Tunisia anashikilia nafasi ya kwanza barani Afrika katika mashindano ya ATP na WTP.

Alimaliliza wa pili katika mashindano ya Wimbledon mwaka 2022 na 2023 na pia kwenye US Open ya mwaka 2022 akiweka historia kuwa mwafrika na mwarabu wa kwanza kufika fainali ya mashindano hayo makubwa ya tenisi.   

“Tunajivunia sana kuwa na Ons Jabeur. Ameipa motisha kizazi kipya,” anaongezea Salma Mouelhi, rais wa tenisi nchini Tunisia.  

Salma anafichua kuwa timu yote ya ukocha ya Ons ni raia kutoka Tunisia. Kocha wake anaitwa Karim Kamoun ni mumewe wa ndoa.  

“Mimi kama rais mpango wangu ni kupata wachezaji wengi bora, kwa hivyo hua tunaandaa mashindano ya wiki 52, ili kuboresha wachezaji wetu katika msimamo wa dunia,” Salma. 

Tunisia pia ndio wenyeji wa akademia ya Afrika ambayo huleta pamoja wachezaji bora 24 kutoka Afrika.   

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.