Pata taarifa kuu
BURUNDI-UN

Maandamano dhidi ya Umoja wa Mataifa yafanyika mjini Bujumbura

Warundi wasiozidi mia moja wameandamana Alhamisi hii, Septemba 22 mbele ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Bujumbura, wakilaani ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini humo.

Maandamano yaliyopangwa na serikali katika mji wa Bujumbura dhidi ya Ufaransa na azimio la Umoja wa Mataifa Julai 30, 2016.
Maandamano yaliyopangwa na serikali katika mji wa Bujumbura dhidi ya Ufaransa na azimio la Umoja wa Mataifa Julai 30, 2016. STR / AFP
Matangazo ya kibiashara

Waandamanaji, miongoni mwao walikuwa Watutsi na Wahutu, makabila makuu nchini Burundi, wameelezea kwamba ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa imejaa uongo na uzushi. Ripoti ya Umoja wa Mataifa imeonya kuwa huenda kukatokea nchini Burundi mauaji ya kimbari, iwapo jumuiya ya kimataifa haitokua makini, kwa hali inayoendelea kushuhudiwa nchini Burundi.

"Hakuna kudanganywa", "Hakuna mauaji ya kimbari nchini Burundi", hayo ni baadhi ya maneno waliyokua wakiyatamka waandamanaji hao.

"Tumekuja kuonyesha hasira zetu dhidi ya ripoti ya Umoja wa Mataifainayothibitisha kwamba mauaji ya kimbari yamo mbioni kutokea hapa nchini Burundi. uchunguzi huu si wa kweli", ameshutumu mmoja wa waandamanaji.

Ripoti hiyo iliyotolewa wiki hii inamtuhumu vikosi vya usalama vya Burundi kuwa vilihusika katika "mauaji kwa kiasi kikubwa."

Wachunguzi huru wa Umoja wa Mataifa walioendesha uchunguzi huo wanabaini kwamba tishio la mauaji ya kimbari liko katika kiwango cha juu nchini Burundi.

Serikali ya Burundi imeelezea kuwa ripoti hiyo imeandikwa kwa "shinikizo la kisiasa".

"Ripoti hiyo inasema ukweli. Inaonyesha ukweli ambao raia wa Burundi wanapitia," amesema mmoja wa waangalizi wa siasa ya Burundi.

"Kwa ujumla, waandishi wa ripoti hiyo wana taarifa zote. Wamekua wakiuliza watu wengi," ameongeza.

Hayo yakijiri Wizara ya Mambo ya Ndani imewataka Wakuu wa mikoa na viongozi wa tarafa, kwa ushirikiano na vikosi vya usalama, kila mmoja katika eneo analoongoza, kuandaa maandamano Jumamosi wiki hii dhidi ya Umoja wa Mataifa kwa kulaani ripoti ya umoja huo kuhusu hali ya haki za binadamu nchini humo.

Machafuko yaliyosababisha vifo vya watu wengi yalitokea nchini Burundi kufuatia uamuzi wa Rais Pierre Nkurunziza, mwezi Aprili mwaka 2015, wa kuwania muhula mwingine wa urais.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.