Pata taarifa kuu
HAKI-SHERIA

Mtuhumiwa wa ubakaji, akiwa pia mpinzani wa Rwanda Christopher Kayumba aachiliwa huru

Kiongozi wa upinzani nchini Rwanda, Christopher Kayumba, yuko huru tangu Jumatano wiki hii baada ya kuachiliwa huru mjini Kigali akishtakiwa kwa ubakaji na kuzuiliwa kwa miezi 17.

Christopher Kayumba alikamatwa Desemba 10, 2019.
Christopher Kayumba alikamatwa Desemba 10, 2019. Getty Images
Matangazo ya kibiashara

Profesa huyu wa chuo kikuu mwenye umri wa miaka 49 alikamatwa Septemba 2021 na kisha kushtakiwa kwa ubakaji na kushiriki ubakaji baada ya shutuma zilizotolewa dhidi yake na watu kadhaa, akiwemo aliyekuwa mwanafunzi wake wa chuo kikuu, kulingana na Ofisi ya Uchunguzi ya Rwanda.

Bw. Kayumba, ambaye alianzisha gazeti la mtandaoni liitwalo "The Chronicles", alizindua chama cha kisiasa cha upinzani dhidi ya Rais Pul Kagame mnamo mwezi Machi 2021. Muda mfupi baadaye, tuhuma za kwanza za ubakaji, ambazo alikuwa amepinga, ziliibuka kwenye mitandao ya kijamii. Siku ya Jumatano, mahakama ya Kigali ilimwachilia huru kwa mashtaka yote, ikisema ushahidi uliotolewa "hautoshi".

"Mahakama inamwona Bw Kayumba kuwa hana hatia katika makosa yote na inaagiza aachiliwe mara moja," mahakama ilisema. Mwendesha mashtaka wa umma alikuwa ameomba kifungo cha miaka 10 jela kwa Bw. Kayumba, ambaye hakuwepo wakati hukumu hiyo ilipotangazwa.

Mnamo 2021, Bw. Kayumba aligoma kula kwa siku 11 kupinga tuhuma hizi, akisema "zinazochochewa kisiasa". Alihitmisha mgomo wake wa kula baada ya siku 11 kwa sababu ya "hali yake ya afya ilikuwa imezorota kwa kasi kutokana na kisukari na kuweka maisha yake hatarini", ameeleza wakili wake.

Mpinzani huyo alikamatwa mwezi Desemba 2019, na kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela kwa "kuhatarisha usalama", mamlaka ilihakikisha kwamba alikuwa amefika kwenye uwanja wa ndege wa Kigali akiwa amechelewa kwa safari kwenda Nairobi na alikuwa amelewa, na kwamba alikuwa ametishia " kufunga uwanja wa ndege".

Mwaka jana, mwajiri katika chama cha Bw. Kayumba alihukumiwa kifungo cha miaka 10 jela baada ya kushtakiwa kwa kuanzisha kundi la uhalifu. Tangu kumalizika kwa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, ambayo yalisababisha vifo vya watu 800,000 hasa Watutsi, Rwanda imetawaliwa kwa mkono wa chuma na Paul Kagame.

Akisifiwa kwa mafanikio ya sera yake ya maendeleo, rais kwa upande mwingine anakosolewa na mashirika ya haki za binadamu kwa ukandamizaji wake hasa wa uhuru wa kujieleza.

Nchi hiyo imeorodheshwa ya 136 kati ya nchi 180 kwa uhuru wa vyombo vya habari na shirika la Wanahabari Wasio na Mipaka (RSF). Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, vyombo vya habari huru vimekuwa adimu, vikikandamizwa na mamlaka, ikiwa ni pamoja na vile vya mtandaoni.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.