Pata taarifa kuu

Zimbabwe: El Nino yazua wasiwasi mkubwa wa raia kukumbwa na nja

Mfumo wa Hali ya hewa, El Nino, inazua sintofahamu, huku wasiwasi wa njaa ukitanda kwa mamilioni ya Wazimbabwe.

Kutokana na ukame unaotishia raia, Rais Emmerson Mnangagwa ameahidi kuwa hakuna Mzimbabwe atakayekufa kwa njaa.
Kutokana na ukame unaotishia raia, Rais Emmerson Mnangagwa ameahidi kuwa hakuna Mzimbabwe atakayekufa kwa njaa. © AFP
Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu milioni 13 kusini mwa Afrika wanakosa chakula na idadi hii inatarajiwa kuongezeka katika miezi ijayo huku matokeo ya miezi kadhaa ya ukosefu wa mvua yakionekana.

Nchini Zimbabwe, mamlaka imewataka watu kukaza mikanda yao: "Familia zinapaswa kupunguza gharama. Ni lazima wawe makini na waandae chakula kinachohitajika kwa kila mlo," ameshauri Leonard Munamati, mkuu wa shirika la serikali linalotoa ushauri wa kilimo na maendeleo vijijini.

Rais Emmerson Mnangagwa ameahidi kuwa hakuna Mzimbabwe atakayekufa kwa njaa. Lakini Ladias Konje anasema kwamba tayari, kama wengine wengi, watoto wake huenda shuleni kila asubuhi wakiwa hawajapata kifungua kinywa. Shamba la tumbaku, ambalo kwa kawaida humuwezesha kupata pesa kidogo, pia halijazaa matunda mengi kama ilivyotarajiwa.

"Familia zinategemea kuchuma matunda mwitu," ameonya Mbunge Tendai Nyabani, alipotembelea Kanyemba, ngome ya chama cha ZANU-PF kilichoko madarakani tangu uhuru wa nchi hiyo mwaka 1980. Baadhi yao sasa wamelazimika kutengeneza unga kutokana na mbegu zilizowekwa kemikali ambazo awali zilikusudiwa kupandwa, afisa aliyechaguliwa amebaini.

"Nafaka za GMO"

Serikali inasaidiwa na shirika moja lisilo la kiserikali na Umoja wa Mataifa kupeleka misaada. Na upinzani ulitaka kutopendelea ngome za ZANU-PF wakati wa usambazaji, jambo ambalo serikali imekuwa ikilaumiwa huko nyuma.

Mamlaka pia inafikiria kuongeza uagizaji wa chakula kutoka nje. Lakini El Nino, ambayo husababisha sehemu kubwa ya Pasifiki ya kitropiki kuwa na joto na kusababisha joto la juu kote ulimwenguni, pia inaleta uharibifu katika nchi jirani. "Kwa kawaida tulinunua mahindi ya asili kutoka Zambia. Leo Zambia haina mahindi na wala Malawi haina nafaka hiyo," anasema Tafadzwa Musarara, mkuu wa Chama cha Wasagaji wa Zimbabwe.

Mwezi Februari, hali ya maafa ilitangazwa nchini Zambia kutokana na ukame. "Sasa sote tunanunua mahindi ya GMO kutoka Afrika Kusini," anaendelea Bw. Musarara. Uagizaji wa nafaka zilizobadilishwa vinasaba uliletwa tena nchini Zimbabwe mwaka 2020 wakati wa ukame mwaka uliyopita.

Pamoja na matatizo ya ugavi, bei pia zimepanda, na hivyo kuchochea mfumuko wa bei unaozidi kupanda kwa kasi. Kanyemba na maeneo jirani, gunia la kilo 25 la mahindi sasa linaweza kugharimu hadi dola 15. Haiwezekani kumudu katika nchi ambayo asilimia 42 ya watu wanaishi katika umaskini uliokithiri kwa chini ya dola 2.15 kwa siku, kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani.

Sekta ya kilimo ya Zimbabwe ilidhoofishwa sana na mageuzi ya ardhi yaliyozinduliwa na Robert Mugabe baada ya uhuru, na kutimuliwa kwa maelfu ya wakulima wa Kizungu kugawa tena ardhi kwa wakulima weusi wasio na vifaa na mafunzo ya kutosha.

Serikali sasa inawahimiza wakulima kuelekeza mazao kwenye nafaka sugu kama vile mtama na inategemea ujenzi wa mabwawa mawili yaliyozinduliwa mwaka wa 2018 katika mkoa wa Kanyemba lakini ambayo yamechelewa kutokana na janga la UVIKO. "Kwa kukamilika kwa mabwawa haya mawili, tutakuwa na suluhisho endelevu katika suala la maji na uzalishaji wa chakula," anatumai Mbunge Nyabani.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.