Pata taarifa kuu
ALGERIA

Rais wa zamani wa Algeria Abdelaziz Bouteflika aaga dunia

Televisheni ya serikali ya Algeria imetangaza kifo cha rais wa zamani wa nchi hiyo Abdelaziz Bouteflika. Alifariki Ijumaa hii akiwa na umri wa miaka 84.

Rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika Juni 15, 2015 huko Algiers.
Rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika Juni 15, 2015 huko Algiers. AFP PHOTO / POOL / ALAIN JOCARD
Matangazo ya kibiashara

Habari ya kifo cha Abdelaziz Bouteflika ilitangazwa na runinga ya taifa ya Algeria, ikinukuu taarifa kutoka ofisi ya rais wa Jamhuri: "Kifo cha rais wa zamani Abdelaziz Bouteflika" iliandikwa kwenye bango jekundu lililokuwa likipitishwa mara kwa mara kwenye runinga ya taifa Ijumaa jioni.

Tangu aachie ngazi baada ya shinikizo kutoka kwa jeshi na maandamano ya kiraia, rais wa zamani wa Algeria alikuwa akiishi katika nyumba yake huko Zeralda, magharibi mwa Algiers. Televisheni za serikali zilitangaza tu kifo cha rais Abdelaziz Bouteflika, bila hata hivyo kukatiza programu zao ili kutoa matangazo maalum kufuatia tukio hilo.

Waziri kijana

Abdelaziz Bouteflika alizaliwa mnamo mwaka 1937 huko Oujda, Morocco, ambapo baba yake alihamia akiwa bado kijana, lakini hakuisahau nchi ya wazazi wake. Wakati mnamo mwaka 1956, katikati ya vita vya Algeria, wanaharakati waliokuwa wakitetea uhuru wa Algeria waliwataka wanafunzi wajiunge na vuguvugu linalopigania ukombozi, Abdelaziz Bouteflika alijiunga haraka na vuguvugu la FLN. Baadae aliteuliwa kuwa katibu wa kibinafsi wa Kanali Boumédiène.

Mnamo mwaka 1962, alikuwa na miaka 25 tu wakati Algeria ilipopata uhuru. Abdelaziz Bouteflika aliteuliwa kuwa Waziri wa Vijana na kisha Waziri wa Mambo ya Nje, na wakati huo alikuwa waziri kijana zaidi katika wadhifa huu duniani. Alihudumu kwa miaka 16.

Baada ya kifo cha kiongozi wake Houari Boumédiène, aliondolewa katika kisiasa, akashtakiwa kwa ubadhirifu wa mali ya umma. Abdelaziz Bouteflika aliondoka nchini na kukimbilia uhamishoni nchini Uswisi na Umoja wa Falme za Kiarabu, hadi aliporudi Algeria mnamo 1987.

Mnamo mwaka 1999 alichukuwa madaraka kwa msaada wa jeshi. baada ya kuondoa pingamizi na wapinzani wake wote.

Muhula wa tano ni miaka mingi mno

Alifikia madaraka ya uongozi wa nchi akiwa na umri wa miaka 62 wakati nchi yake ilikuwa ilikumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vilisababisha vifo vya watu kati ya 90,000 na 150,000. Abdelaziz Bouteflika aliahidi kumaliza fitna na mafarakano. Watu 6,000 walijisalimisha na silaha zao, mivutano ilipungua, ingawa ugaidi haukukomeshwa kabisa.

Baada ya mihula miwili, alibadilisha Katiba, ambayo ilimruhusu kusalia madarakani kwa muhula wa tatu, kisha muhula wa nne ambao aliuanza akitembea kwa kutumia kiti cha magurudumu, baaada ya kupata ugonjwa kiharusi mnamo 2013.

Baada ya kutangaza nia yake ya kuwania kwa muhula wa tano, maandamano ambayo hayajawahi kutokea yalifanyika nchini na kusababisha kuundwa kwa vuguvugu la "Hirak". Baada ya kuonekana kuwa ni dhaifu na afya yake inaendelea kuzorota, Abdelaziz Bouteflika alilazimishwa kujiuzulu na mkuu wa jeshi Aprili 2, 2019, baada ya wiki sita za maandamano makubwa ya kiraia. Siku hiyo alionekana kwa mara ya mwisho kwenye runinga akitangaza kwamba anaachia ngazi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.