Pata taarifa kuu
EQUATORIAL GUINEA-CAN2015

Nchi ya Equatorial Guinea kuwa mwenyeji wa michuano ya AFCON 2015

Nchi ya Equatorial Guinea imekubali kuwa mwenyeji wa michuano ya kombe la mataifa ya Afrika kwa mwaka 2015 baada ya nchi ya Morocco ambayo ilikuwa iwe mwenyeji wa mashindano haya makubwa barani Afrika kukataa kuandaa kutokana na hofu ya ugonjwa wa Ebola.

Rais wa shirikisho la mpira wa miguu barani Afrika CAF, Issa Hayatou.
Rais wa shirikisho la mpira wa miguu barani Afrika CAF, Issa Hayatou. AFP PHOTO / FADEL SENNA
Matangazo ya kibiashara

 

Juma lililopita shirikisho la mpira wa miguu barani Afrika, CAF lilitangaza kuiondoa nchi ya Morocco kama mwenyeji wa michuano ya mwakani kutokana na uongozi wa nchi hiyo kukataa kuwa mwenyeji kwa kile ilichodai hofu ya kuenea kwa virusi vya Ebola.

Hatua ya Morocco kujiondoa kama mwenyeji wa michuano ya mwakani ya CAN, iliifanya CAF kuanza upya harakati za kusaka nchi ambayo itakubali kuwa mwenyeji wa michuano hiyo kwa tarehe iliyokuwa imepangwa ambapo sasa nchi ya Equatorial Guinea imekubali kuwa mwenyeji.

Kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari rais wa CAF, Issa Hayatou amesema kuwa baada ya kuwa na mazungumzo ya kina na rais wa Equatorial Guinea, Teodore Obian'g Nguema hatimaye kiongozi huyo alikubali nchi yake kuwa mwenyeji wa mashindano ya hapo mwakani yanayotarajiwa kuanza january 17 hadi February 8 mwaka 2015.

Nchi ya Equatorial Guinea inakubali kuwa mwenyeji wa mashindano haya licha ya tishio la ugonjwa wa Ebola ambao umeyakumba mataifa mengi ya ukanda wa Afrika Magharibi hali ambayo hata hivyo licha ya ugonjwa huo kuanza kudhibitiwa bado kuna hatari kuwa huenda wakati wa michuano hiyo watu wakaambukizwa.

Rais wea CAF, Issa Hayatou anataka nchi ya Morocco ifungiwe kujihusisha na shirikisho hilo kwa muda wa miaka minne kutokana na kunyang'anywa kuwa mwenyeji wa michuano hiyo baada ya kukataa kuandaa.

Morocco haitashiriki michuano ya hapo mwakani, ambapo uamuzi huu pia unaifutia adhabu nchi ya Equatorial Guinea ambayo iliondolewa wakati wa michuano ya kufuzu baada ya kumchezesha mchezaji ambaye hakustahili.

Mwaka wa 2011 nchi ya Equatorial Guinea kwa kushirikiana na Gabon waliandaa kwa pamoja michuano hii ambayo ilifana kwa sehemu kubwa na kuna matumaini kuwa licha ya muda mdogo ambao nchi hiyo inao itahakikisha inaandaa vema viwanja vyake tayari kwa mashindano.

Miongoni mwa viwanja vitakavyotumika ni pamoja na uwanja wa taifa wa mjini Bata wa Estadio de Bata wenye uwezo wa kuchukua mashabiki elfu 35 na mia 7, uwanja mwingine ni ule wa klabu ya The Panters wa mjini Malabo Nuevo Estadio de Malabo wenye uwezo wa kuchukua mashabiki elfu 15.

Uwanja mwingine ni ule wa klabu ya Atletico Malabo “Estadio Internacional wenye uwezo wa kuchukua mashabiki elfu 6, huku uwanja mwingine ukiwa ni ule wa Estadio La Paz wenye uwezo wa kuchukua mashabiki elfu 10.

Kiwanja kingine ambacho kinatarajiwa kutumika ni kile cha Estadio Manuel Enguru na uwanja wa Estadio La Libertad mjini Malabo.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.