Pata taarifa kuu
AFCON 2015

Ratiba ya michuano ya awali ya kufuzu kombe la mataifa ya Afrika nchini Morocco mwaka 2015 yatolewa

Ratiba ya michuano ya awali ya kufuzu kucheza fainali za kombe la mataifa ya Africa (AFCON) kwa mwaka 2015 nchini Morocco hatimaye imewekwa wazi mwishoni mwa juma hili kwenye makao makuu ya shirikisho la mpira barani Afrika CAF, jijini Cairo, Misri.

cafonline.com
Matangazo ya kibiashara

Ratiba hiyo imeshuhudia mabingwa watetezi timu ya taifa ya Nigeria ikipangwa kundi moja na timu ya taifa ya Afrika Kusini katika zile timu saba zinazowania kufuzu kucheza fainali za hapo mwakani.

Kwa upande wa mahasimu wa Afrika Kaskazini, vinara Tunisia waoa watapambana na majirani zao Misri wakati Ghana wao watakuwa na kibarua dhidi ya Togo, huku Ivory Coast wao wakiwakaribisha mabingwa wa siku nyingi timu ya taifa ya Cameroon.

Timu tatu ambazo zilifuzu awali zimepangwa katika kila kundi ambapo timu ya nne itatokana na ile michuano ya awali ya kufuzu.

Rais wa shirikisho la mpira barani Afrika CAF, Issa Hayatou
Rais wa shirikisho la mpira barani Afrika CAF, Issa Hayatou RFI/David Kalfa

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, mzunguko wa kwanza utazikutanisha timu ya taifa ya Liberia dhidi ya Lesotho, wakati Kenya wao watakuwa wenyeji wa timu ya taifa ya visiwa vya Comoro, huku Madagascar wao watawakaribisha timu ya taifa ya Uganda.

Kwenye mchuano mwingine, timu ya taifa ya Mauritania wao watakuwa wenyeji wa Equatorial Guinea, wakati Namibia watakuwa wenyeji wa Congo, huku Libya wakiwakaribisha nyumbani timu ya taifa ya Rwanda.

Mechi nyingine za mzunguko wa kwanza utazikutanisha timu ya taifa ya Burundi watakaokuwa wenyeji wa timu ya taifa ya Botswana, wakati Jamhuri ya Afrika ya Kati wao watakuwa wenyeji wa Guinea Bissau, huku Gambia wao wakiwakaribisha timu ya taifa ya visiwa vya Seychelles.

Mechi nyingine ni kuwa timu ya taifa ya Sao Tome watakuwa wenyeji wa Benin, wakati Malawi watakuwa wenyeji wa Chad huku timu ya taifa ya Tanzania wakliwa wenyeji wa timu ya taifa ya Zimbabwe na Msumbiji wao watakuwa wenyeji wa timu ya taifa ya Sudan Kusini.

Mechi hizi za mzunguko wa kwanza zitachezwa kuanzia tarehe 16 na 18 ya mwezi May na mechi za marejeano zitapigwa tarehe 30, 31 May na tarehe 1 ya mwezi June mwaka 2014 ambapo timu zitakazopata ushindi zitafuzu kwenye mzunguko wa pili.

Mechi za mzunguko wa pili wa michuano hii ya kufuzu kucheza kombe la mataifa ya Afrika kwa mwaka 2015 utazikutanisha timu ya taifa ya Liberia au Lesotho watakaocheza na mshindi kati ya timu ya taifa ya Kenya au Comoro.

Mechi nyingine ni mshindi kati ya timu ya taifa ya Uganda au Madagascar ambaye atacheza na mshindi kati ya timu ya taifa ya Mauritania au Equatorial Guinea, huku mshindi kati ya Namibia au Congo akitarajhiwa kukutana na mshindi kati ya Libya au Rwanda.

Mshindi kati ya Burundi au Botswana atakutana na mshindi kati ya Jamhuri ya Afrika ya Kati au Guinea Bissau, huku mshindi kati ya Swaziland au Sierra Leone atakutana na mshindi kati ya Gambia au Seychelles.

Rais wa chama cha soka cha Zambia, Kalusha Bwalya akishangilia kombe na wachezaji wa timu yake ya taifa mwaka 2012
Rais wa chama cha soka cha Zambia, Kalusha Bwalya akishangilia kombe na wachezaji wa timu yake ya taifa mwaka 2012 cafonline.com

Mshindi kati ya timu ya taifa ya Sao Tome e Principe au Benin atakutana na mshindi kati ya Malawi au Chad, huku mshindi kati ya Tanzania au Zimbabwe atakutana na mshindi kati ya Mozambique au South Sudan.

Michuano hii ya mzunguko wa pili itapigwa kati ya tarehe 18 na 20 ya mwezi July mwaka huu na zile mechi za marudiano zitachezwa kati ya tarehe 1 na 3 ya Mwezi August mwaka huu na washindi katika mechi hizo watakuwa wamejikatia tiketi ya kuingia kwenye makundi ya timu zitakazocheza fainali za mwaka 2015.

Michuano ya kombe la mataifa ya Afrika kwa mwaka 2015 nchini Morocco itapigwa kuanzia tarehe 17 ya mwezi January hadi tarehe 8 ya mwezi February.

Miji ya Marrakech, Agadir, Rabat na Tangier viwanja vyake vitatumika kwenye fainali hizi, ambapo mji wa Marrakech uwanja wake utatumika kwa mechi ya ufunguzi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.