Pata taarifa kuu
KENYA-SIASA-RAILA ODINGA

Kenya: Upinzani wajiondoa kushiriki uchaguzi wa marudio

Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga, ametangaza kuwa hatashiriki katika Uchaguzi mpya wa urais uliopangwa kufanyika tarehe 26 mwezi huu.

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya (NASA)  Raila Odinga
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya (NASA) Raila Odinga REUTERS/Thomas Mukoya
Matangazo ya kibiashara

Odinga na mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka, wamesema kuwa hawawezi kushiriki katika Uchaguzi huo bila kuwepo kwa mabadiliko ndani ya Tume ya Uchaguzi.

Aidha, ameeleza kuwa, uamuzi huu umefikiwa kwa ajili ya wananchi wa taifa hilo ili kuwepo kwa mabadiliko yatakayowezesha Uchaguzi kuwa huru na haki.

Tayari amemwandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Wafula Chebukati kuelezea uamuzi huu.

Odinga amekuwa akieleza kuwa, hatashiriki katika Uchaguzi uliopangwa iwapo Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Uchaguzi Ezra Chiloba hatajiuzulu lakini pia iwapo wabunge wa Jubilee wataendelea kuifanyia marekebisho sheria ya Uchaguzi.

Muungano wa upinzani NASA, umetaka Tume ya Uchaguzi kufanya uteuzi mpya wa wagombea urais na kutoendelea na Uchaguzi wa tarehe 26 kama ilivyopangwa.

Uamuzi huu, umezua mvutano zaidi ya kisiasa nchini humo, kwa sababu unamwacha rais Uhuru Kenyatta peke yake kama mgombea baada ya Uchaguzi wa mwezi Agosti kufutwa na Mahakama ya Juu.

Tume ya Uchaguzi inatarajiwa kutoa mwelekeo kuhusu hatima ya Uchaguzi huo mpya , huku baadhi ya wachambuzi wakisema kuwa uchaguzi uliopangwa unastahili kufutwa kwa mujibu wa Katiba.

Katiba inaeleza kuwa iwapo kutakuwa na wagombea wawili na mmoja ajiondoe, basi Uchaguzi uliopangwa hautakuwepo.

Wakati uo huo, muungano wa NASA umesema utaendelea kuwa na maandamano ya kila wiki kushinikiza mabadiliko ndani ya Tume ya Uchaguzi kabla ya Uchaguzi mwingine kufanyika.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.