Rais wa Sudan na makamu wake wafikia makubaliano ya kuunda jeshi la pamoja
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na Makamu wake Riek Machar wamekubaliana kuunda jeshi la pamoja ikiwa ni hatua kubwa ya kutekeleza mkataba wa amani wa mwaka 2018.
Imechapishwa:
Kiir na Machar, wamekubaliana kuunda jeshi la pamoja, moja ya masuala muhimu ambayo yamekuwa yakileta utata, na kusababisha kutotekelezwa kikakamilifu kwa mkataba huo wa amani uliolenga kuleta utulivu nchini humo.
Martin Abucha, aliyesaini makubaliano hayo kwa niaba ya upande wa upinzani wa Machar, amesema amani inahusu usalama na kwamba hii ni hatua waliyoipiga ya kufungua mwanya wa kuwa na serikali imara ya Sudan Kusini.
Kwenye makubaliano hayo Upande wa rais Kiir utachukua asilimia 60 huku ule wa Machar ukichukua asilimia 40 katika nyadhifa muhimu za uongozi wa jeshi, polisi na vikosi vingine vya usalama vya taifa.
Hatua hii imekuja wiki moja baada ya kuwa na wasiwasi wa kutokea kwa mapigano kati ya vikosi vya rais Kiir na vile vya Machar na kuzua wasiwasi wa kuzuka kwa vita vingine kama ilivyokuwa kati ya mwaka 2013 hadi 2018.