Pata taarifa kuu
RWANDA

Maadhimisho ya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari yaanza Rwanda

Hii leo nchini Rwanda wananchi wa taifa hilo wanaanza maadhimisho ya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi na wahutu wenye msimamo wa wastani ambapo inakadiriwa watu milioni moja waliuawa kwa kipindi cha siku 100.

Picha hii ya zamani iliyopigwa tarehe 7 Aprili, 2000 inaonyesha wafanyakazi kutoka timu moja ya wachimbaji 50, wanaondoa mabaki ya watu waliouawa katika mauaji ya kimbari kwenye kaburi la halaiki huko Nyamirambo karibu na Kigali, Rwanda
Picha hii ya zamani iliyopigwa tarehe 7 Aprili, 2000 inaonyesha wafanyakazi kutoka timu moja ya wachimbaji 50, wanaondoa mabaki ya watu waliouawa katika mauaji ya kimbari kwenye kaburi la halaiki huko Nyamirambo karibu na Kigali, Rwanda Marco Longari/AFP
Matangazo ya kibiashara

Haya ni maadhimisho ya 27 tangu kutokea kwa mauaji hayo, ambapo mwaka huu nchini Rwanda yanafanyika tofauti na mwaka jana.

Hakukuwa na ratiba yoyote maalum kutokana na kuongezeka kwa maambukizi ya Virusi vya Corona, lakini mwaka huu baada ya kasi ya maambukizi kupungua na sasa siku hii ya maadhimisho ya kitaifa hii leo Jumatano, maafisa wachache watakusanyika kwenye Kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbari ya Kigali iliyoko Gisozi kuwasha moto wa matumaini ambao utaanza shughuli za ukumbusho.

Hafla ya kitaifa imepangwa kufanyika katika uwanja wa Kigali na itakusanya maafisa tofauti na wawakilishi wa makundi tofauti ya watu kama vile wanadiplomasia, manusura wa mauaji ya kimbari, wanawake, vijana, viongozi wa dini, sekta binafsi na wengine.

Kagame kulihutubia taifa

Katika hafla hiyo, Rais Paul Kagame anatarajiwa kutoa hotuba kuu na hii, kama shughuli zote zilizopangwa zitaonyeshwa mubashara kupitia runinga ya taifa na kupitishwa moja kwa moja kwenye majukwaa mengine ya mitandao ya kijamii.

Mauaji hayo ya Kimbari nchini Rwanda yalianza tarehe kama ya leo siku moja baada ya kudunguliwa kwa ndege ya aliekuwa rais wa nchi hiyo katika anga la uwanja wa ndege wa Kanombe Juvenal Habyarimana aliyekuwa ameambatana na rais wa Burundi Cyprien Ntaryamira na mawaziri wake wawili Cyriaque Simbizi na Bernard Ciza.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.