Pata taarifa kuu
USALAMA-AFYA

Zaidi ya mia moja wafariki katika ajali ya boti nchini Msumbiji

Msako umendelea Jumatatu katika pwani ya Msumbiji baada ya vifo vya takriban watu 96 kufuatia kuzama kwa boti ya wavuvi iliyojaa mizigo, ambapo familia nyingi zilizojawa na hofu zilikimbia baada ya uvumi wa janga la kipindupindu.

Boti ya wavuvi kwenye pwani ya Msumbiji (picha ya kielelezo).
Boti ya wavuvi kwenye pwani ya Msumbiji (picha ya kielelezo). Getty Images - Eddie Gerald
Matangazo ya kibiashara

"Miili mingine mitano imepatikana katika muda wa saa chache zilizopita, na kufanya idadi ya waliofariki kufikia 96," Silverio Nauaito, msimamizi wa kisiwa kidogo katika jimbo la kaskazini la Nampula, ameliambia shirika la habari la AFP siku ya Jumatatu asubuhi. Ripoti ya hapo awali Jumapili iliripoti vifo vya angalau watu 91. Boti hiyo ya wavuvi ilikuwa imebeba watu wapatao 130, ikiwa ni pamoja na watoto wengi, ilipozama mapema Jumapili jioni. Watu 11 walionusurika wamehesabiwa lakini idadi ya watu wanaotafutwa bado haijajulikana.

"Idadi ya waliotoweka bado haijulikani, kwa sababu mwanzoni tulijua kwamba kulikuwa na watu 130 kwenye boti, (...) hii ni data ambayo lazima tuchunguze kwa usahihi," amesema Bw Nauaito, akisema kwamba baadhi ya maaiti ziiombwa na familia. "Miili ya mwisho kutambuliwa ni ya watoto watatu," amesema msimamizi wa kisiwa cha Msumbiji, chenye jina linalofanana na la nchi, na ambapo boti ilikuwa ikielekea.

Picha zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha makumi ya miili iliyofunikwa na blanketi ikiwa imelalazwa ufukweni. "Boti ilizama kwa sababu ilikuwa imejaa kupita kiasi na haikufaa kusafirisha abiria," Jaime Neto, katibu wa Jimbo la Nampula, alielezea Jumapili jioni.

Abiria wengi walikuwa wakijaribu kukimbia eneo hilo kutokana na taarifa za uongo kuhusu ugonjwa wa kipindupindu unaoendelea, jambo ambalo lilizua hofu, Neto alisema, bila kufafanua.

Kipindupindu na wanajihadi

Msumbiji, mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani, imerekodi karibu kesi 15,000 za ugonjwa huu unaosambazwa na maji machafu, na watu 32 wamefariki tangu mwezi wa Oktoba, kulingana na takwimu rasmi. Mkoa wa Nampula ndio mkoa ulioathirika zaidi, ukizingatia theluthi moja ya kesi. Katika miezi ya hivi karibuni, pia umepokea watu wengi waliokimbia makazi yao wanaokimbia mfululizo wa mashambulizi ya wanajihadi katika mkoa jirani wa Cabo Delgado, kaskazini mwa nchi.

Uchunguzi umefunguliwa ili kubaini sababu za kuzam kwa boti hiyo, amesema Waziri wa Mambo ya Nje, na kuongeza kuwa manusura kadhaa wamelazwa hospitalini.

Kisiwa cha Msumbiji, ambacho kilikuwa mji mkuu wakati wa ukoloni wa Ureno, ni kituo cha biashara cha zamani kwenye njia ya kwenda India. Nchi hiyo, ambayo ina ufuo wa takriban kilomita 2,500 kwenye Bahari ya Hindi, imekuwa huru tangu 1975. Kisiwa hiki, ambacho ni makazi ya jiji lenye ngome kilomita nne tu kutoka bara hilo, kimeorodheshwa kuwa eneo la urithi wa dunia wa UNESCO.

Nchi hiyo, ambayo ina wakazi zaidi ya milioni 30, hukumbwa mara kwa mara na vimbunga haribifu. Huku takriban theluthi mbili ya watu wakiishi chini ya mstari wa umaskini, Msumbiji imeweka matumaini makubwa katika hifadhi kubwa ya gesi asilia iliyogunduliwa huko Cabo Delgado mwaka 2010.

Lakini vita vya msituni vilivyoongozwa tangu mwaka 2017 na wanajihadi wenye silaha wanaohusishwa na kundi la Islamic State vimestisha uchimbaji wa gesi hiyo. Zaidi ya watu 5,000 wameuawa na karibu milioni moja wamelazimika kukimbia makazi yao tangu kuanza kwa mzozo huu. Kampuni ya mafuta ya TotalEnergies, ambayo wakati huo iliitwa Total, ilisimamisha mradi mkubwa mnamo mwezi Machi 2021 baada ya shambulio kubwa la wanajihadi, ambalo lilisababisha wahanga - idadi bado haijulikani - kati ya wakazi wa eneo hilo na kati ya wakandarasi wake wadogo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.