Pata taarifa kuu

Tunisia yawarejesha wahamiaji 400 katika nchi zao za asili

Takriban wahamiaji 400 kutoka Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara "waliokwama nchini Tunisia" wamerudishwa makwao katika siku za hivi karibuni katika nchi walizotoka, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) ambalo liliwezesha operesheni hii limetangaza Ijumaa.

Wahamiaji kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara wamekamatwa katika ufuo wa jiji la Tunisia la Sfax, katika Bahari ya Mediterania, na mamlaka ya Tunisia walipokuwa wakijaribu kuelekea pwani ya Italia, Oktoba 4, 2022.
Wahamiaji kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara wamekamatwa katika ufuo wa jiji la Tunisia la Sfax, katika Bahari ya Mediterania, na mamlaka ya Tunisia walipokuwa wakijaribu kuelekea pwani ya Italia, Oktoba 4, 2022. © Fethi Belaid / AFP
Matangazo ya kibiashara

 

Jumla ya watu 392, hususan raia wa Burkina Faso, Gambia, Mali na Senegal, walinufaika na "utaratibu wa kurejea kwa hiari kwa usalama na heshima kamili", imeeleza IOM katika taarifa yake. Baada ya kuwasili katika nchi zao, watapokea "msaada wa kuunganishwa upya ili kujenga upya maisha yao na kujiunga na familia zao," kulingana na taarifa kwa vyombo vya habari.

Mnamo mwaka wa 2023, IOM ilisaidia "wahamiaji 2,557 kurejea kwa hiari kutoka Tunisia hadi nchi zao za asili", yaani 45% zaidi ya mwaka wa 2022. IOM imebainisha kuwa inafanya kazi "kwa ushirikiano wa karibu na serikali ya Tunisia" na wawakilishi wake wa ndani ikitaja maeneo ya Sfax (katikati-mashariki), kitovu cha uhamiaji haramu kutoka Tunisia hadi Ulaya, pamoja na Médenine na Tataouine, maeneo mawili ya kusini mwa Tunisia.

Katika kipindi cha miezi 11 ya kwanza ya mwaka 2023, Tunisia ilinasa karibu wahamiaji haramu 70,000, zaidi ya mara mbili ya idadi ya mwaka 2022, kulingana na kikosi cha walinzi wa kitaifa. Kati ya jumla hii, 77.5% walikuwa wageni, wengi wao wakiwa raia kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara, na wengine Tunisia, ikilinganishwa na 59% ya wageni mnamo 2022.

Kuondoka kwa raia wa Kusini mwa Jangwa la Sahara kuliongezeka kwa kasi nchini Tunisia baada ya hotuba mwishoni mwa mwezi wa Februari na Rais Kais Saied, akilaani kuwasili kwa "makundi ya wahamiaji haramu" ambao alikuwa amewaonyesha kama tishio la idadi ya watu kwa nchi yake.

Kulingana na ripoti ya Shirika la Kupambana na Mateso Duniani (OMCT) iliyochapishwa katikati ya mwezi wa Desemba, wahamiaji, wakimbizi na wanaotafuta hifadhi nchini Tunisia wanateseka "ghasia za kila siku za kitaasisi", "kukamatwa kiholela", "kuhamishwa kwa nguvu" na "kufukuzwa kinyume cha sheria" kuelekea mpaka na Libya na Algeria.

Ripoti hiyo ilitaja "ukiukwaji mwingi wa haki za binadamu", huku ikibainisha kuwa nchi hiyo iko chini ya "shinikizo linaloendelea kutoka Ulaya ili kupunguza uhamiaji haramu katika Bahari ya Mediterania". Utafiti huo pia ulishutumu "kutokuwa na uwezo wa mamlaka ya Tunisia kuwalinda" watu hawa, ikionyesha "hali zisizofaa za maisha, bila kupata huduma za msingi, ajira na vyanzo vya mapato".

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.