Pata taarifa kuu

Kipindupindu chapungua kwa 37% barani Afrika lakini mafuriko huongeza hatari ya kusambaa

Idadi ya wagonjwa wapya wa kipindupindu barani Afrika imepungua kwa asilimia 37 wiki iliyopita, ikiongezeka kwa kasi mwanzoni mwa mwaka, lakini mafuriko kusini mwa Afrika yana hatari kubwa ya kusababisha kusambaa kwa ugonjwa huo, ofisi ya kanda ya Shirika la Afya Duniani (WHO) imesema siku ya Alhamisi.

Kituo cha matibabu ya kipindupindu wilayani Tete, Msumbiji, Machi 5, 2015 (picha ya zamani).
Kituo cha matibabu ya kipindupindu wilayani Tete, Msumbiji, Machi 5, 2015 (picha ya zamani). AFP PHOTO/Mauricio Ferretti
Matangazo ya kibiashara

Kesi mpya zilishuka hadi 2,880 katika wiki iliyoishia Februari 26, chini ya 37% kutoka wiki iliyopita wakati kesi 4,584 zilirekodiwa, amesema Dk Matshidiso Moeti, mkurugenzi wa WHO kwa Afrika, wakati wa mkutano wa waandishi wa habari. Hata hivyo, amesema, idadi ya vifo "haijabadilika", ikishuka kutoka 82 hadi 81 katika kipindi hicho.

Katika taarifa yake, WHO inabainisha kuwa mafuriko makubwa kutokana na mvua za msimu na vimbunga vya kitropiki kusini mwa Afrika huongeza hatari ya ugonjwa huo kuenea na kutishia kudhoofisha juhudi za kudhibiti janga hilo. Kulingana na WHO, visa vya ugonjwa wa kipindupindu kwa sasa vinaripotiwa katika nchi kumi na mbili za Afrika, ikiwa ni pamoja na Malawi "ambayo inakabiliwa na janga baya zaidi la kipindupindu katika historia yake".

Katika nchi hii, "kuongezeka kwa mvua kunapunguza juhudi za kudhibiti mlipuko katika baadhi ya maeneo, huku timu za kukabiliana na hali hiyo zikihangaika kuwafikia watu wanaohitaji kutokana na barabara mbovu na miundombinu iliyoharibika. Baadhi ya vituo vya matibabu ya kipindupindu vimekumbwa na mafuriko," kulingana na WHO.

Nchini Msumbiji, iliyokumbwa na dhoruba ya kitropiki Februari 24, ugonjwa wa kipindupindu unaathiri majimbo sita kati ya 11, kulingana na WHO. Nchi imekubwa na ongezeko kubwa la wagonjwa tangu Desemba 2022. Chanjo inaendelea kutolewa.

Nchini Madagascar, ugonjwa wa kipindupindu uliripotiwa mara ya mwisho mwaka 2000. Lakini vimbunga vilipiga kisiwa hicho mnamo mwezi Januari na Februari na kusababisha mafuriko, ambayo yalisababisha kuzuka tena kwa ugonjwa wa Malaria na kuongeza hatari ya milipuko ya kipindupindu, amesema Profesa Zely Arivelo Randriamanantany, Waziri wa Afya wa Madagascar.

"Tunaimarisha usaidizi wetu kwa nchi ili kuongeza uwezo wa kutambua magonjwa, kuwasilisha vifaa vya matibabu na kuimarisha maandalizi katika maeneo yaliyo katika hatari ya mafuriko," Dk Moeti amesema.

Wakati wa mkutano wake wa kila wiki mnamo Februari 9, WHO-Afrika ilishtushwa na "ongezeko kubwa" la idadi ya wagonjwa wa kipindupindu barani Afrika, ambao katika mwezi wa kwanza wa 2023 walifikia zaidi ya 30% ya jumla ya idadi ya kesi zilizorekodiwa 2022.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.