Pata taarifa kuu

CAR: Maxime Mokom, kiongozi wa Anti-balaka akabidhiwa ICC

Maxime Mokom, kiongozi wa kundi la wanamgambo wa Kikristo la Anti-balaka alihamishwa kutoka Chad na kupelekwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu Jumatatu.

Wawakilishi wa makundi yenye silaha wakati wa kutia saini mkataba wa Khartoum mjini Bangui, Machi 3, 2019. Miongoni mwao, Souleymane Daouda (wa 3 kushoto) na Maxime Mokom (wa kwanza kulia).
Wawakilishi wa makundi yenye silaha wakati wa kutia saini mkataba wa Khartoum mjini Bangui, Machi 3, 2019. Miongoni mwao, Souleymane Daouda (wa 3 kushoto) na Maxime Mokom (wa kwanza kulia). RFI/Gaël Grilhot
Matangazo ya kibiashara

Maxime Mokom alikamatwa mwishoni mwa Februari nchini Chad. Kiongozi huyu anashitakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita, uliofanywa mwaka 2013 na 2014 nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Maxime Mokom alikuwa chini ya hati ya kukamatwa, iliyotolewa dhidi yake na majaji wa ICC mnamo Desemba 2018. Miezi mitatu baadaye, aliteuliwa kuwa Waziri mwenye dhamana ya kuwapokonya silaha waasi, licha ya tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita, iliyotolewa na mwendesha mashtaka.

Orodha ya uhalifu anaotuhumiwa ni ndefu: mauaji, ukatili, mateso, visa vya watu kutoweka kwa lazima, ukeketaji, unyanyasaji ... na mengi mengi. Kulingana na taarifa ya mahakama, anti-balaka inadaiwa kutekeleza mashambulizi dhidi ya watu kutoka jamii ya Waislamu, wanaoshukiwa kuwa washirika wa kundi la zamani la Seleka. Seleka ambayo ilikuwa imempindua Rais François Bozizé mwaka 2013, ambaye Maxime Mokom ni mshirika wake wa karibu.

Maxime Mokom ni afisa wa nne kutoka Jmahuri ya Afrika ya Kati kukabidhiwa mahakama ya ICC. Anamkuta jela Patrice-Edouard Ngaïssona, mratibu wa zamani wa kisiasa wa kundi la Anti-Balaka, ambaye kesi yake bado inaendelea mbele ya ICC. Maxime Mokom ataonekana kwa mara ya kwanza mbele ya majaji wa Mahakama ya ICC katika siku zijazo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.