Pata taarifa kuu
UCHAGUZI ZAMBIA

Lungu atangazwa mshindi wa uchaguzi mkuu wa Rais nchini Zambia

Tume ya uchaguzi nchini Zambia imemtangaza Edgar Lungu wa chama tawala cha PF, kuwa mshindi wa kinyang'anyiro cha uchaguzi mkuu wa Urais uliofanyika Alhamisi iliyopita kwa kupata asilimia 50.35 ya kura zote.

Rais wa Zambia, Edgar Lungu, ambaye amefanikiwa kutetea nafasi yake kwenye uchaguzi wa Alhamisi, Agosti 11, 2016
Rais wa Zambia, Edgar Lungu, ambaye amefanikiwa kutetea nafasi yake kwenye uchaguzi wa Alhamisi, Agosti 11, 2016 DR
Matangazo ya kibiashara

"Namtangaza Rais Edgar Lungu kuwa mshindi wa kiti cha Urais wa Zambia," alisema Esau Chulu mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi, baada ya kusoma matokeo rasmi ya kura zote, yanayompa ushindi rais Lungu kwa zaidi ya kura laki moja mbele ya mpinzani wake wa karibu, Hakainde Hichilema.

Matokeo haya yamepingwa tayari na mgombea wa upinzani wa chama cha UPND, Hakainde Hichilema, ambaye amelalamikia kuhusu uwepo wa udanganyifu wakati wa uhesabuji kura.

Siku ya Jumapili, Hichilema akiongozana na wafuasi wake, walifika kwenye makao makuu ya tume ya uchaguzi ya Zambia ambako matakeo yanatangaziwa akitaka kukutana na mwenyekiti wa tume, lakini hata hivyo alizuiliwa na Polisi.

Hichilema anadai kulikuwa na udanganyifu mkubwa wa kura kwenye jimbo la Lusaka na maeneo mengine ya nchi, ambako anasema tume ya uchaguzi ilichelewa kutangaza matokeo yake kwa kuwa yalikuwa yakitengenezwa ili kumpa ushindi Rais Lungu ambaye anatetea kwa mara nyingine nafasi yake.

Uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa wa upinzani mkali kati ya Rais Lungu, ambaye pia alimshinda hichilema kwenye uchaguzi wa mwaka jana kwa kura elfu 28, na safari hii mchuano ulikuwa mkali zaidi kutokana na upinzani ulioshuhudiwa.

Hata hivyo wadadisi wa mambo wanaamini kuwa uchaguzi wenyewe ulikuwa na mapungufu, ikiwemo vitisho kwa baadhi ya maofisa wa tume, lakini kwa sehemu kubwa wanakubaliana kuwa ulifanyika kwa huru na haki.

Waangalizi wengi wa kimataifa kwenye ripoti zao za awali waliwapongeza wananchi wa Zambia kwa kushiriki uchaguzi kwa amani licha ya dosari ndogondogo ambazo walizibaini ingawa hawasema ikiwa uchaguzi ulikuwa wakuaminika.

Wananchi wa Zambia sasa huenda wakaondoa hofu iliyokuwepo awali kuhusu uwezekano wa kutokea machafuko.

Wakati akihitimisha kampeni zake Rais Lungu aliahidi kuilinda katiba ya nchi kwa kuhakikisha usalama wa raia dhidi ya watu waliodaiwa kutaka kufanya vurugu.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.