Pata taarifa kuu
NIGERIA-BOKO HARAM-MASHAMBULIZI

Nigeria: zaidi ya watu 30 wauawa katika mashambulizi ya kujitoa mhanga

Mashambulizi mawili ya kutjitoa mhanga yameendeshwa na wanawake mapema Jumatatu hii asubuhi katika soko la jimbo la Adamawa, kaskazini mashariki mwa Nigeria, chanzo cha kijeshi kimetangaza, wakati ambapo kiongozi mmoja katika jimbo hilo amesema kuwa watu zaidi ya thelathini wameuawa.

Picha iliopigwa wakati wa mashambulizi ya Boko Haram karibu na mji wa Gombe, Nigeria, mwezi Februari mwaka 2015.
Picha iliopigwa wakati wa mashambulizi ya Boko Haram karibu na mji wa Gombe, Nigeria, mwezi Februari mwaka 2015. AFP PHOTO/AMINU ABUBAKAR
Matangazo ya kibiashara

Mkuu wa kijeshi katika jimbo la Adamawa, Victor Ezugwu, amethibitisha kwamba mashambulizi mawili ya kujitoa mhanga yalitokea katika mji wa Madagali bila hata hivyo kueleza hasara iliyosababishwa na mashambulizi hayo.

"Wanawake wawili waliojitoa mhanga wamewaua watu wasiopungua 30 katika milipuko miwili iliyotokea katika soko", Maina Ularamu, mkuu wa zamani wa serikali ya eneo la Madagali ameliambia shirika la habari la Ufaransa la AFP.

Mapema Jumatatu, mwanamke amejilipua wakati watu walipokuwa wakijiandaa kuingia Msikitini.

Hayo yakijiri watu zaidi ya 20 wameuawa katika mashambulizi zaidi ya matatu yalioendeshwa Jumapili usiku na watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa Boko Haram katika mji wa Maiduguri, nchini Nigeria.

Watu wengi wameuawa baada ya kijiji cha Dawari na vitongoji vyake kushambuliwa na watu waliokua wamejihami kwa bunduki Jumapili usiku.

Hata hivyo jeshi limebaini kwamba liliwaua wapiganaji 10 walioshukiwa kuwa washambuliaji wa kujitoa mhanga.

Chanzo cha polisi kimesema katika muda wa saa 24, mashambulio manne ya kujitoa mhanga yametekelzwa, na yote yaliendeshwa na wanawake.

Mji wa Maiduguri wakati mmoja ulichukuliwa kuwa ngome kuu ya wapiganaji wa Boko Haram.

Hivi karibuni Boko Haram imezidisha mashambulio ya kujitoa mhanga katika mji wa Maiduguri na maeneo mengine kaskazini mwa Nigeria.

Kundi hili la Boko Haram linanatumia wanawake vijana wa umri mdogo kwa kutekeleza mashambulizi ya kujitoa mhanga.

Hivi karibuni rais wa Nigeria Muhammadu Buhari alipongeza majeshi yake na kusema kuwa yalikuwa yamewashinda wapiganaji wa Boko Haram, huku akibaini kwamba wapiganaji wa kundi hilo hawawezi tena kuendesha mashambulizi katika maeneo yenye wakazi wengi, hususan mijini na katika kambi za jeshi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.