Pata taarifa kuu
SUDAN-SUDAN KUSINI

Sudan na Sudan Kusini zaafikiana kuanza uzalishaji wa mafuta

Sudan Kusini imetia saini makubaliano ya kuanza kwa oparesheni ya uzalishaji mafuta kupitia bomba la Sudan, hatua hiyo inakuja ikiwa ni mwaka mmoja umepita tangu serikali ya Juba itangaze kusitisha oparesheni zote za uzalishaji mafuta kupitia Sudan.

REUTERS/Stuart Price/United Nations Mission in Sudan/Handout
Matangazo ya kibiashara

Makubaliano hayo yameshuhudiwa na mpatanishi wa Umoja wa Afrika AU ambaye ni Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Juba na Khartoum utekelezaji wa oparesheni hiyo utaanza katika kipindi cha majuma mawili yajayo.

Majirani hao wawili wamekuwa katika hali tete kiuchumi tangu Juba isitishe oparesheni za mafuta mwaka mmoja uliopita ikiishutumu Khartoum kuiba rasilimali zake.

Suala la biashara ya mafuta na mgogoro wa mipaka limekuwa likitatiza makubaliano baina ya mataifa hayo mawili na utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua.

Tayari majeshi kutoka pande zote yalisema yamekubali kuondoa wanajeshi wao kwenye mpaka wenye mgogoro ingawa bado kumeendelea kuwa na hofu iwapo utekelezaji wake utafanikiwa.

Sudan Kusini ilipata uhuru wake toka kwa Sudan mwezi julai 2011 huku watu takribani milioni moja na nusu wakidhaniwa kupoteza maisha katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.