Pata taarifa kuu
DRC-UGANDA-UCHIMI-USALAMA

Felix Tshisekedi azungumza na wawekezaji kutoka DRC, Kampala

Katika ziara ya kiserikali ya siku mbili katika mji mkuu wa Uganda, Kampala, Rais wa DRC Felix Tshisekedi amekutana na wafanyabiasha na wadau wote katika uchumi wa DRC kutoka katika mikoa ya Kivu Kusini, Kivu Kaskazini na Ituri.

Rais wa DRC Felix Tshisekedi amefanya ziara ya siku mbili nchini Uganda. Hapa alikuwa Entebbe, Novemba 9, 2019.
Rais wa DRC Felix Tshisekedi amefanya ziara ya siku mbili nchini Uganda. Hapa alikuwa Entebbe, Novemba 9, 2019. © Sumy Sadurni / AFP
Matangazo ya kibiashara

Rais Tshisekedi amewapokea wadau katika uchumi wa DRC, Novemba 10, wakati wa mkutano uliolenga kuboresha uchumi kati ya DRC na Uganda.

Wadau hao katika uchumi nchini DRC wameweza kuelezea matatizo yao katika suala la usalama, ushuru na mambo mengine yanayokabiliana nayo katika shughuli zao.

Wajumbe kutoka mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri wote wamesisitiza kuhusu matatizo ya ukosefu wa usalama ambayo yamekuwa na changamoto kubwa katika shughuli za kiuchumi nchini DRC na katika nchi jirani.

Felix Tshisekedi ameahidi ka mara nyingine kuanzisha vita dhidi ya makundi yenye silaha, hasa yale yanayotatiza usalama kwenye barabara zinazoelekea nchini Uganda, mashariki mwa DRC. Pia amezungumzia kuhusu hali inayojiri katika mji wa Minembwe, mkoani Kivu Kusini, ambapo ametaja kuwa "hali ya usalam katika eneo hilo inatisha".

Lakini ukosefu wa usalama sio kikwazo pekee kwa shughuli ya biashara nchini DRC, hasa Mashariki mwa nchi hiyo.

Wadau katika uchumi wa DRC pia wamelalamikia kuhusu hali ya barabara. Wameomba ujenzi wa barabara zinazounganisha miji ya Komanda na Mahagi na Komanda-Kisangani, lakini pia kukarabati uwanja wa ndege wa Bunia, hali ambayo inaweza kutoa mwelekeo mwingine wa kuimarisha biashara na Uganda, wamesema. Rais Tshisekedi amewahakikishia kuwa amezungumzia sula hilo na viongozi na wawekezaji kutoka Uganda.

Wafanyabiashara pia wamemzungumzia rais Tshisekedi kuhusu shida za kiutawala na matatizo ya kodi wanayokumbana nayo.

Umekuwa ni mkutano wa kwanza wa kibiashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili, na kuhudhuria rais Felix Tshisekedi akiambatana na ujumbe wa watu 117 wakiwemo Mawaziri.

Miongoni mwa mambo yaliyokubaliwa katika mkutano huo ni kwa Kampala na Kinshasa kushirikiana katika masuala ya miundo mbinu, biashara na uwezekaji pamoja na ulinzi na usalama.

Katika mkutano huo, rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema, anaunga mkono ombi la DRC kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuungana na mataifa mengine kama Kenya, Uganda, Tanzania, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini.

Uhusiano wa Uganda na DRC katika miaka iliyopita, ulionekana kuwa mbaya lakini tangu kuingia madarakani kwa rais Tshisekedi mwezi Januari, mambo yameanza kubadilika huku nchi hizo mbili zikiahidi kushirikiana zaidi.

Baada ya ziara yake nchini Uganda, rais Tshisekedi amekwenda jijini Paris kukutana na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.