Pata taarifa kuu

Ukraine: Watu saba wameuawa katika shambulio la Urusi

Nairobi – Watu saba wakiwemo watoto watatu wameuawa katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Urusi kwenye kituo cha petroli katika mji wa Kharkiv mashariki mwa Ukraine.

Shambulio la Urusi katika kituo cha mafuta nchini Ukraine
Shambulio la Urusi katika kituo cha mafuta nchini Ukraine AFP - SERGEY BOBOK
Matangazo ya kibiashara

Kupitia mtandao wake wa Telegram, gavana wa eneo hilo Oleg Synegubov amethibitisha tukio hilo.

Aidha gavana huyo ameeleza kuwa miongoni mwa watu waliouawa ni watoto watatu wenye umri wa miaka 7 na 4 na mtoto mwengine mwenye umri wa karibia miezi sita.

Naye meya wa Kharkiv Igor Terekhov amesema karibia watu 50 waliokuwa wanaishi karibu na kituo hicho cha petroli wamelazimika kuhama makazi yao kutokana na shambulio hilo.

Shambulio hili linakuja wakati huu rais Zelensky akifanyia mageuzi idara yake ya jeshi
Shambulio hili linakuja wakati huu rais Zelensky akifanyia mageuzi idara yake ya jeshi AP - Efrem Lukatsky

Mwendesha mashtaka wa mkoa wa Kharkiv, Oleksandr Filachkov naye ameeleza kwamba ndege zisizo na rubani tatu zilishambulia wilaya ya Nemyshlyanskyi katika mji wa Kharkiv.

Kando na vifo, miundombinu muhimu pia imeripotiwa kuharibiwa kutokana na moto uliosababisha na kiasi kikubwa cha mafuta kilichokuwa kwenye kituo hicho cha mafuta kilichoshambuliwa.

Shambulio hilo la siku ya Jumamosi limekuja wakati huu Urusi ikiendelea kutekeleza mashambulizi huko Kharkiv na kijiji kilicho mashariki mwa mji mkuu wa mkoa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.