Uchaguzi Ujerumani: Chama cha mrengo wa kati kushoto cha SPD chaibuka mshindi
Nchini Ujerumani, chama cha siasa za mrengo wa kati kushoto, SPD, kimepata ushindi mwembaba dhidi ya muungano wa kihafidhina wa CDU na CSU ambao umekuwa ukiongozwa na Kansela Angela Merkel anayemaliza muda wake.
Imechapishwa:
Matokeo ya awali ya uchaguzi uliofanyika siku ya Jumapili, yanaonesha kuwa chama cha SPD kimepata ushindi mwembamba wa asilimia 25.7 na kukushinda chama cha Kansela Merkel cha CDU ambacho kimeibuka katika nafasi ya pili kwa asililia 24.1.
Chama cha SPD kinaongoza kwa asilimia mbili zaidi, wakati huu matokeo ya mwisho yanaposubiriwa.
Tayari kiongozi wa chama cha SPD Olaf Scholz amejitokeza na kusema matokeo yanaonesha kuwa, chama chake kimeshinda na kupewa nafasi ya kuongoza nchi hiyo ya bara Ulaya.
Naye Armin Laschet, kiongozi wa chama cha CDU licha ya kuwa nyuma, ana imani kuwa atafanikiwa kuunda serikali na kumrithi Kansela Merkel ambaye uongozi wake wa miaka 16 unafika mwisho. Hii ndio mara ya kwanza baada ya muda mrefu chama cha CDU kinapata matokeo mabaya.
Kufuatia vyama vya SDP na CDU/CSU, kuonesha nia ya kuunda serikali kutokana na uchaguzi huu wenye ushindani mkali, upande wowote unaweza kufanya hivyo, iwapo utapata washirika wanaohitajika kuunda serikali ya muungano.
Iwapo hali itakuwa hivyo, Kansela Merkel ataendelea kuongoza hadi pale serikali ya muungano itakapoundwa labda kufikia baadaye mwezi Desemba.