Pata taarifa kuu
CATALONIA-UHISPANIA-HAKI

Catalonia yatishia kutangaza uhuru wake

Nchini Uhispania, wakati ambapo imesalia siku moja tu ili taasisizi zote za jimbo la Catalonia kuwa chini ya mamlaka ya serikali kuu ya Madrid, mvutano bado unaendelea.

Waandamanaji wanadai jimbo la Catalonia kuwa huru, Barcelona, Jumatano, Oktoba 25, 2017.
Waandamanaji wanadai jimbo la Catalonia kuwa huru, Barcelona, Jumatano, Oktoba 25, 2017. REUTERS/Rafael Marchante
Matangazo ya kibiashara

Rais wa Catalonia, Carles Puigdemont, alifutilia mbali mwaliko wa kuzungumza siku ya Alhamisi mbele ya bunge la Seneti ambalo litaamua kuhusu kusimamishwa kwa kujitawala kwa Catalonia siku ya Ijumaa Oktoba 27.

Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy, kwa upande wake, amesema Catalonia kuwa chini ya mamlaka ya Madrid ni "njia moja pekee inayowezekana" dhidi matarajio ya uhuru.

Mvutano unaendelea kuongezeka kati ya serikali kuu ya Uhispania na serikali ya Catalonia. Kila upande unashtumu mwengine kukataa mazungumzo.

Madrid inaandaa kuchukua udhibiti wa jimbo la Catalonia chini ya Ibara ya 155 ya Katiba. Bunge la Seneti litakutana katika kikao maalum siku ya Ijumaa na litapitisha hatua kali ambazo zitaanza kutumika siku ya Jumamosi Oktoba 28. Serikali ya Catalonia itafutwa. Utawala na polisi vitakua chini ya mamlaka ya serikali kuu ya Uhispania. kwa upande wa bunge la Seneti la jimbo hilo, litasimamishwa hadi utakapofanyika uchaguzi mpya.

Wakati huo huo viongozi wa Catalonia wametishia kutangaza uhuru wa jimbo lao siku ya Ijumaa wakati ambapo bunge la Seneti litapitisha azimio la serikali kuu la kudhibiti taasisi zote za jimbo hilo.

Wanaharakati wa upinzani katika jimbo la Catalonia wanapanga kufanya maandamano ya kushinikiza kujitenga kwa eneo hilo.

Jitihada za kuwashawishi viongozi wa eneo hilo kuachana na mpango wa kujitangazia uhuru wa eneo hilo baada ya kuwa na kura ya maoni na kujitenga wiki kadhaa zilizopita zinaendelea.

Serikali ya Madrid imesema, haiwezi kutambua uhuru wa eneo hilo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.