Pata taarifa kuu
Tong Il-Moo-Do

Kenya yaanza vyema mashindano ya Tong Il Moo Do, Mombasa nchini Kenya

Mombasa, Kenya – Timu ya taifa ya Kenya 'Jasiri' iko mbioni kuhifadhi ubingwa wa mashindano ya kimataifa ya Mombasa Open Tong-Il-Moo-Do kwa miaka 11 mfululizo katika ukumbi wa Akademia ya Aga Khan mjini Mombasa kufuatia kuanza vizuri katika siku mbili za kwanza za mashindano.

Mchezaji wa Kenya wa Tong Il Moo Do kwenye hafla ya kuonyesha mbinu na sifa zake
Mchezaji wa Kenya wa Tong Il Moo Do kwenye hafla ya kuonyesha mbinu na sifa zake © Kenya Tong Il Moo Do Federation media
Matangazo ya kibiashara

Michuano hiyo ilianza Jumapili usiku kwa hotuba ya ufunguzi iliyorekodiwa mapema na mwanzilishi wa sanaa ya kijeshi, mchungaji Sun Myung Moon kabla ya mashabiki kutumbuizwa katika shindano la kuonyesha umahiri wa mbinu za wachezaji iliyohusisha misururu ya miondoko.

Kasisi Moon alisema:

Inanipa furaha sana kuungana nanyi kwa toleo hili la Mashindano ya Mombasa Open Tong Il Moo Do. Nawatakia washiriki wote uzoefu mzuri wanaposhindana wao kwa wao.

Wachezaji wa Tong Il Moo Do kwenye sherehe ya ufunguzi ya Mombasa Open mnamo 17/12/2023
Wachezaji wa Tong Il Moo Do kwenye sherehe ya ufunguzi ya Mombasa Open mnamo 17/12/2023 © Kenya Tong Il Moo Do Federation media

Rais wa shirikisho la Tong Il Moo Do barani Afrika na nchini Kenya, Clarence Mwakio aliahidi kueneza mchezo huo kote nchini katika misimu miwili ijayo akidai wamepokelewa vyema katika maeneo mengi na huo ni mwanya mzuri wa kuanzia kuuza sera za mchezo huo kote kote. 

Wakenya waliofanya vyema zaidi usiku huo ni pamoja na Joseph Daud (pointi 9.00), Trevor Wanjiku (pointi 8.60) na Mohammed Shaban (pointi 8.90).

Wachezaji wengine waliokuwa uwanjani ni pamoja na Jambia Ali (pointi 6.30), Harrington Wanjala (pointi 5.80) na Sudi Mohammed (pointi 5.00).

Ushindani mkuu ulishuhudiwa siku ya Jumatatu jioni wakati wa mashindano ya sparring kwenye vitengo tofauti vya umri. 

Flevian Kemunto, Hope Cristine, Hassan Zulpha, Bakari Mwanasheban waliongoza kwenye vitengo vyao katika fainali hizo za sparring. Hata hivyo raia kutoka India Erica de Sequeira, 13, alimbwaga mkenya alimbwaga Eunice Mwende 3-2 na kujitangaza zaidi baada ya kutumbuiza uwanja awali kupitia densi ya mziki wa kizazi kipya.

Erica de Sequeira, 13, kutoka India baada ya ushindi wake dhidi ya mkenya Eunice Mwende mnamo 18/12/2023
Erica de Sequeira, 13, kutoka India baada ya ushindi wake dhidi ya mkenya Eunice Mwende mnamo 18/12/2023 © Jason Sagini

Clarence Mwakio alisema timu nyingi zilifanya vyema siku ya kwanza ambayo ilikuwa kupima sifa na mbinu za timu katika mafunzo na msingi wa sparring. Hata hivyo, alisisitza kuna haja ya wachezaji wachanga kupata mafunzo zaidi ili kuboresha ujuzi wao.

Hatua yenye upinzani ilianza jana, lakini leo itakuwa kubwa zaidi kwenye michuano ya timu za wakubwa. Kuwa tayari kwa mihemko katika hafla ya watu wazima. Tunatazamia timu kama Iran, na Zambia kurudisha ushindani wao baada ya pambano la mwaka jana. Lakini Kenya walianza vizuri sana na nina imani tutatetea ubingwa.

Kenya inalenga kuhifadhi taji waliloshinda mwaka jana ambapo Kenya ilishinda jumla ya medali 185 katika vitengo tofauti.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.