Pata taarifa kuu
Tong Il-Moo-Do

Tong-Il-Moo-Do yakua haraka Afrika kuelekea Mombasa Open wikendi hii

Mombasa, Kenya – Rais wa shirikisho la Kimataifa la mchezo wa Tong Il Moo Do, Takamitsu Hoshiku amesifia juhudi za bara la Afrika katika ukuzaji wa mchezo huo barani, akidai wachezaji wa Afrika wanajifunza kwa haraka sana kwa kushika mbinu kadhaa haraka.

Timu ya taifa ya Kenya ya Tong Il Moo Do kwenye mazoezi ukumbini Light International School, Mombasa nchini Kenya 16/12/2023
Timu ya taifa ya Kenya ya Tong Il Moo Do kwenye mazoezi ukumbini Light International School, Mombasa nchini Kenya 16/12/2023 © Jason Sagini
Matangazo ya kibiashara

Rais huyo alikuwa akizungumza siku ya Jumamosi katika ukumbi wa mazoezi wa Light International School baada ya kukamilisha mazoezi ya jioni na wachezaji. 

Wachezaji wa Afrika wako vizuri kwenye kurusha teke na makonde, na sasa wanajifunza haraka sana mbinu zingine kama mizunguko ya mikono. Nimevutiwa sana nao. Wanaweza kutumia mbinu hizo kujikinga ila nafurahia sana wanavyozidi kuimarika.

Rais wa Tong Il-Moo-Do nchini Kenya, Clarence Mwakio alimshukuru sana rais Hoshiku kuwa nao kwa wiki mbili zilizopita akikiri wamejifunza mengi.

Tunafurahia sana kwa shirikisho la kimataifa kutuwezesha kuandaa tena mashindano haya.

Mashindano yaliyopita ya Tong-Il-Moo-Do jijini Mombasa
Mashindano yaliyopita ya Tong-Il-Moo-Do jijini Mombasa © https://www.tongilmoodokenya.com/

Mji wa Mombasa utaandaa mashindano ya Mombasa Open kuanzia Jumapili ya tarehe 17 hadi Jumatatu tarehe 18 huku jumla ya mataifa 21 tu kati ya 4é yaliyoalikwa yakitarajiwa kushiriki. Tayari, Ufilipino, Thailand, Paraguay, Korea, India, Japan, Zimbabwe na DRC zimewasili mjini Mombasa.

Changamoto kubwa ni kuwa wakati huu ndege ni chache na wasafiri ni wengi kutoka mataifa mengi ambayo tulialika - Clarence Mwakio, rais wa Tong Il-Moo-Do nchini Kenya.

Awali mashindano haya yalifaa kuanza Ijumaa tarehe 15 mwezi Disemba lakini yakaahirishwa hadi Jumapili baada ya serikali kukosa kutoa ufadhili kwa wakati. Clarence Mwakio alidhibitisha na kutoa shukranI kwa kupokea ufadhili wa $642,948 kutoka kwa wizara ya michezo nchini Kenya kufadhili mashindano na timu ya taifa ya Kenya 'Jasiri'.

Jasiri inalenga kutetea ubingwa ambao wameushinda katika makala yote kumi yaliyopita. Master Mwakio amesema timu hiyo iko imara na dhabiti kupambana na wenzake kuhakikisha taji inasalia nchini Kenya.

Mara nyingi Ufilipino hua inatupa upinzani mkali lakini tuko nyumbani na mashabiki wetu wapo kwa hivyo naamini bado tuna uwezo wa kutetea ubingwa.

Timu ya taifa ya Kenya ya Tong Il Moo Do kwenye mazoezi ukumbini Light International School, Mombasa nchini Kenya 16/12/2023
Timu ya taifa ya Kenya ya Tong Il Moo Do kwenye mazoezi ukumbini Light International School, Mombasa nchini Kenya 16/12/2023 © Jason Sagini

Aidha Mwakio alielezea ukuaji wa kasi kwa mchezo huo nchini Kenya huku wakilenga kueneza mchezo huo katika kaunti zote 47. Shirikisho hilo linalenga kutumia shule za msingi kama kitovu cha kukuza mchezo huo. Baada ya mwaka 2024, watalenga kupeleka mafunzo katika shule za upili ili kuzalisha wakufunzi zaidi ambao wataendelea kuwafunza watoto wa shule za msingi. 

Mashindano ya msimu huu yana lengo tofauti la kukuza utalii katika ukanda wa Pwani ya Kenya. Mechi zitaanza saa kumi na moja jioni hadi saa nne usiku katika ukumbi wa Akademia ya Agha Khan. 

Kwa mujibu wa rais wa shirikisho la kimataifa Takamitsu Hoshiku, wanalenga kuhahakikisha katika siku zijazo mchezo huo ni sehemu ya Michezo ya Olimpiki.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.