Pata taarifa kuu
WAFCON 2016

AFCON 2016 Wanawake: Nigeria, Ghana zatoka sare, Kenya yakubali kipigo cha Mali

Michuano ya kombe la mataifa ya Afrika kwa upande wa wanawake imeshika kasi nchini Cameroon, ambako tayari baadhi ya timu zitakazocheza hatua ya robo fainali zimeshajulikana, huku timu hizo zikiwa zimebakiza mechi moja moja.

Wachezaji wa timu ya Nigeria na Ghana wakichuana wakati wa mchezo wao.
Wachezaji wa timu ya Nigeria na Ghana wakichuana wakati wa mchezo wao. Cafonline.com
Matangazo ya kibiashara

Jumatano ya wiki hii mechi za kundi B zilipigwa, zikihusisha timu ya taifa ya Nigeria, Ghana, Mali na Kenya wawakilishi pekee kutokana ukanda wa Afrika Mashariki.

Kattika mechi hizo, Harembee Starlets ambao walikuwa wanahitaji ushindi ili kufufua matumaini yao ya kutinga kwenye hatua ya robo fainali ya michuano ya mwaka huu, walijikuta harakati zao zikigonga ukuta baada ya kukubali kufungwa na wanawake wa Mali.

Kwenye mchezo huo ambao ulikuwa ni wa pili kupoteza kwa timu ya taifa ya wanawake ya Kenya, walikubali kufungwa mabao 3-1 na timu ya taifa ya Mali ambayo kama ilivyokuwa Kenya, ilikuwa inahitaji kupata ushindi ili kujiwekea mazingira mazuri ya kufuzu hatua inayofuata.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Kenya na Mali wakichuana wakati wa mchezo wao wa Afcon
Wachezaji wa timu ya taifa ya Kenya na Mali wakichuana wakati wa mchezo wao wa Afcon Cafonline.com

Timu ya taifa ya Nigeria "Super Falcons" ambao nao walikuwa wanahitaji ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kucheza hatua ya robo fainali, ilijikuta ikilazimishwa sare ya bao 1-1 na timu ya taifa ya Ghana.

Kwa matokeo haya, Nigeria wanaongoza katika kundi B wakiwa na alama 4, sawa na timu ya taifa ya Ghana yenye alama 4 pia.

Mali yenyewe ina alama 3 huku Kenya ikishikilia mkia kwenye kundi hilo ikiwa haina alama yoyote, ambapo hata ikishinda kwenye mchezo wake unaofuatia haitaweza kusonga mbele.

Timu mbili zitakazofuzu kwenye hatua inayofuata kutoka kundi B sasa zitajulikana kwenye mechi za mwisho, ambapo Ghana, Nigeria na Mali zitakuwa zikihitaji ushindi.

Michuano hii inatarajiwa kutimua vumbi Ijumaa ya wiki hii ambapo Zimbabwe itacheza na Cameroon, Misri ikicheza Afrika Kusini huku siku ya Jumamosi Novemba 26, Mali watacheza na Ghana huku Kenya wakitarajiwa kupepetana na Nigeria.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.