Pata taarifa kuu
KENYA-OLIMPIKI 2016

Naibu rais wa Kamati ya Michezo ya Olimpiki nchini Kenya akamatwa

Polisi nchini Kenya wamemkamata Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo ya Olimpiki nchini humo Pius Ochieng.

Mwanariadha Faith Kipyego aliposhinda mbio za Mita 1500 wakati wa Michezo ya Olimpiki 2016 nchini Brazil
Mwanariadha Faith Kipyego aliposhinda mbio za Mita 1500 wakati wa Michezo ya Olimpiki 2016 nchini Brazil Olympic Games 2016
Matangazo ya kibiashara

Hatua hii inakuja baada ya malalamishi mengi kuzuka kutoka kwa wanariadha na raia wa nchi hiyo kuhusu maandalizi mabaya na mazingira magumu ambayo wanariadha walipitia wakati wakishiriki Michezo ya Olimpiki iliyokamilika Agosti 21 nchini Brazil.

Pamoja na changamoto hizo, Kenya ilimaliza ya kwanza barani Afrika na ya 13 duniani, ikiwa na  medali 13, zikiwemo 6 za dhahabu.

Wakati wa Michezo hiyo, Ochieng ndiye aliyekuwa Meneja wa kikosi cha Kenya huko Brazil.

Mbali na Ochieng, viongozi wengine akiwemo Katibu Mkuu wa NOCK Franci K Paul, Mkurugenzi Mkuu wa Kamati hiyo James Chacha na aliyekuwa kiongozi ujumbe wa kikosi cha Kenya Stephen Soi wote walikamatwa na kuhojiwa na polisi na baadaye kuzuiwa ili kufikiswa Mahakamani baada ya msako wa polisi katika Makao makuu wa Kamati hiyo jijini Nairobi.

Kumekuwa na madai kuwa viongozi hao waliweka wanamichezo wa Kenya katika mazingira magumu huku  walioshuhudia wakisema  wanamichezo hao walikuwa wanaishi katika mitaa ya mabanda.

Mbali na hili, inadaiwa kuwa wanariadha hawakupata jezi walizokuwa wametengewa kufanyia mazoezi na badala yake kupewa jezi moja tu.

Suala lingine tata lililojitokeza ni idadi kubwa ya watu ambayo maafisa wa NOCK walipeleka kwenda kushuhudia Michezo hii kama wapenzi wao na watoto huku makocha wa riadha kama John Anzrah wakikosa hata vitambulisho katika Michezo hiyo.

Wiki iliyopita, Waziri wa Michezo Hassan Wario alitangaza kuvunja bodi ya Kamati hiyo ya Olimpiki, huku naye akishinikizwa kujiuzulu.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.