Pata taarifa kuu
OLIMPIKI-BRAZIL 2016-RIADHA

Mo Farah ashinda mbio za Mita 10,000, aweka histria

Mwanariadha Mo Farah ametetea taji lake baada ya kushinda medali ya dhahabu katika mbio za Mita 10,000 kwa upande wa wanaume katika michezo ya Olimpiki inayoendelea nchini Brazil.

Mo Farah alivyoshinda mbio za Mita 10,000
Mo Farah alivyoshinda mbio za Mita 10,000 i.ytimg.com
Matangazo ya kibiashara

Raia huyo wa Uingereza ambaye sasa ameshinda mara mbili katika mbio hizi katika Michezo hii ya Olimpiki mwaka 2012 jijini London na mwaka huu Brazil, alimaliza mbio hizo za kuzunguka uwanja mara 25 kwa muda wa dakika 27 sekunde 05 nukta 17.

Farah ambaye aliangushwa kwa bahati mbaya katika mzunguko wa 10 amesema kushinda mbio hizo haikuwa rahisi, na alipambana kuhakikisha kuwa anatetea taji lake.

Anakuwa mwanariadha wa kwanza wa Uingereza kuwahi kushinda medali tatu za dhahabu katika Michezo ya Olimpiki tangu mwaka 2012 na sasa anasubiri mbio za Mita 5,000 wiki ijayo.

Nafasi ya pili ilimwendea Mkenya, Paul Tanui ambaye ameipa nchi yake medali ya fedha baada ya kumaliza kwa muda wa dakika 27 sekunde 05 nukta 64.

Tanui amesema alijikakamua na kujikaza kumpita Mo Farah lakini, hakufanikiwa ila anajivunia medali aliyoipata.

Nafasi ya tatu ilimwendelea raia wa Ethiopia, Tamirat Tola aliyemaliza kwa muda wa dakika 27 sekunde 06 nukta 27.

Paul Tanui (Kenya,kushoto), Mo Farah (uingereza, katikati na Tamirat Tola (Ethiopia,Kushoto) baada ya kutuzwa medali baada ya mbio za Mita 10,000 nchini Brazil
Paul Tanui (Kenya,kushoto), Mo Farah (uingereza, katikati na Tamirat Tola (Ethiopia,Kushoto) baada ya kutuzwa medali baada ya mbio za Mita 10,000 nchini Brazil Reuters

Hadi tunapochapisha makala haya, Marekani inaongoza kwa medali 60, zikiwemo 24 za dhahabu.

China ni ya pili kwa medali 41, Uingereza ya tatu kwa medali 30.

Ujerumani ni ya nne kwa medali 16 huku Japan ikifunga tano bora kwa medali 24.

Ethiopia ni ya 34 baada ya kupata medali 3, moja ya dhahabu na mbili za shaba.

Afrika Kusini ni ya 44 kwa medali 6, tano za fedha na moja ya shaba.

Kenya ni ya 46 duniani kwa medali 2, zote za fedha.

Ratiba

Jumapili Agosti 14 2016

  • 9:30 Alasiri-Mbio za Marathon kwa wanawake.
  • 9:00 usiku-Nusu fainali Mita 100 kwa upande wa wanaume
  • 9:30 usiku-Nusu fainali Mita 1500 kwa upande wa wanawake.
  • 10:25 Alfajiri-Fainali ya Mita 100 kwa upande wa wanaume.

Jumatatu Agosti 15 2016

  • Saa 10:25 jioni-Mzunguko wa kwanza Mita 3000 kuruka viunzi na maji kwa upande wanaume.
  • Saa 11:15 jioni-Fainali ya mbio za Mita 3000 kuruka viunzi na maji kwa upande wanawake.
  • 10:25 Alfajiri-Fainali ya Mita 800 kwa upande wa wanaume.
  • 10:45 Alfajiri-Fainali ya mbio za Mita 400 kwa upande wa wanawake.
Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.