Pata taarifa kuu
OLIMPIKI-BRAZIL 2016

DRC kuwakilishwa na wanamichezo watatu michezo ya Olimpiki

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo itawakilishwa na wachezaji watatu katika michezo ya Olimpiki inayotarajiwa kuanza tarehe 5 mwezi ujao nchini Brazil.

Mwanariadha wa mbio ndefu za DRC Makorobondo Salukombo
Mwanariadha wa mbio ndefu za DRC Makorobondo Salukombo Dailyrepublic
Matangazo ya kibiashara

Itakuwa ni makala 10 ya DRC kushiriki mara ya kwanza ikiwa ni mwaka- 1968,1984,1988,1992,1996,2000,2004,2008,2012 na sasa 2016.

Wachezaji hao ni pamoja na mwanariadha Makorobondo Salukombo ambaye atashiriki katika mbio za masafa marefu (Marathon) kwa upande wa wanaume.

Makorobondo ndio mwanariadha pekee anayekwenda nchini Brazil kuiwakilisha nchi yake katika mchezo huo.

Ni mwanariadha ambaye amekuwa akiishi nchini Marekani lakini alilazimika kurudi nyumbani na kupiga kambi katika eneo la Kirotshe katika jimbo la Kivu Kaskazini kuendelea na mazoezi yake.

Kwa muda wa miaka minne iliyopita, amekuwa akijiandaa kushiriki katika michezo hii na mwezi Januari alishiriki katika mashindano ya Florida Marathon na kumaliza kwa muda wa saa 1 dakika 4 na sekunde 25, mashindano ambayo yalimsaidia kufuzu katika michezo hiyo.

Rodrick Kuku ni mwanamichezo mwingine atakayewakilisha nchi yake katika mchezo wa Judo.

Kuku alifuzu baada ya kuwa miongoni mwa wachezaji bora kutoka barani Afrika, walioshiriki katika michezo ya dunia ya vijana yaliyofanyika mwezi Mei mwaka huu.

Rosa Keleku ni mwanamke wa pekee atayeiwakilisha nchi yake katika michezo hii katika mchezo wa Taekwondo kwenye uzani wa Kilo 49.

Alifuzu baada ya kumaliza wa kwanza katika mashindano ya kufuzu kwa mataifa ya Afrika yaliyofanyika mjini Aqadir nchini Morocco mwezi Februari mwaka huu.

Keleku anarejesha nchi yake katika michuano hii ya Taekwendo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1996.

Wakati wa michezo ya Afrika iliyofanyika nchini Congo Brazaville mwaka uliopita, Keleku alimaliza wa pili katika mchezo huu na kuongeza nafasi yake ya kufuzu katika michezo hii.

Hadi kufikia michezo ya mwaka huu, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo haijawahi kushinda medali yoyote katika michezo hii, na inakuwa nchi ya pili baada ya Bangladesh kuondoka katika michezo hii mikono mitupu.

Hadi sasa DRC haijawahi kuwa na wanariadha wengi kama ilivyokuwa mwaka 1992 wakati iliofanyika mjini Barcelona nchini Uhispania ilipotuma wanariadha 17.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.