Pata taarifa kuu
USALAMA-ULINZI

Pakistan: Shambulio la bomu laua watu wengi wakati wa mkutano wa kisiasa

Takriban watu 39 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika shambulio la bomu Jumapili Julai 30 kaskazini-magharibi mwa Pakistan wakati wa maandamano ya chama chenye itikadi kali za Kiislamu. Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo hadi sasa, lakini tawi la ndani la kundi la kigaidi la Islamic State (IS) lilidai kuhusika na mashambulizi dhidi ya chama cha kihafidhina.

Gari la wagonjwa likiwabeba hospitalini watu waliojeruhiwa baada ya bomu kulipuka huko Bajur, mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa mnamo Julai 30, 2023.
Gari la wagonjwa likiwabeba hospitalini watu waliojeruhiwa baada ya bomu kulipuka huko Bajur, mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa mnamo Julai 30, 2023. © Rescue 1122 Head Quarters / AP
Matangazo ya kibiashara

 

Mlipuko huo umelenga chama cha kidini cha kihafidhina cha Jamiat Ulema-e-Islam (JUI-F) ambacho zaidi ya wanachama na wafuasi 400 walikuwa wamekusanyika chini ya hema katika mji wa Khar, karibu na mpaka na Afghanistan.

"Ninaweza kuthibitisha kwamba katika hospitali tumepokea miili 39 ya watu walio uawa na watu wengine 123 waliojeruhiwa, ikiwa ni pamoja na 17 wakiwa katika hali mbaya," Riaz Anwar, mwakilishi wa wizara ya afya katika jimbo la Khyber Pakhtunkhwa, ameliambia shirika la habari la AFP. Picha za mlipuko huo zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha miili ikiwa imetapakaa kwenye umati wa watu na watu waliojitolea wakiwasaidia waathiriwa waliojaa damu kingia kwenye gari la wagonjwa.

Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo, lakini tawi la ndani la kundi la Islamic State (IS) hapo awali lilidai kuhusika na mashambulizi dhidi ya JUI-F. Mwaka jana, IS ilisema ilihusika na mashambulizi ya kikatili dhidi ya wasomi wa kidini wenye uhusiano na chama hicho. Chama hiki kina mtandao mkubwa wa misikiti na madrasa (shule za Quran) kaskazini na magharibi mwa nchi.

Kundi hilo la wanajihadi linaishutumu JUI-F kwa unafiki, kwani chama hicho cha kidini kimeunga mkono serikali na wanajeshi.

Serikali ya Pakistan inatazamiwa kuvunjwa katika wiki zijazo kabla ya uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi Oktoba au Novemba, na vyama vya siasa vinajiandaa kufanya kampeni.

Mashambulizi ya mara kwa mara tangu Taliban warudi Kabul

Mashambulizi nchini Pakistan yameongezeka tangu kundi la Taliban kurejea madarakani nchini Afghanistan mwezi Agosti 2021 na kisha kumalizika kwa usitishaji mapigano kati ya kundi la Taliban la Pakistani Tehreek-e-Taliban Pakistan (TTP) na serikali ya Pakistani mwishoni mwa mwezi wa Novemba.

Mashambulizi hayo yanafanyika hasa katika mikoa inayopakana na Afghanistan. Islamabad inabaini kwamba baadhi ya mashambulizi hayo yamepangwa kutoka nchini Afghanistan, madai ambayo Kabul inakanusha. Mnamo Januari, mwanamume, aliyehusishwa na TTP kulingana na mamlaka, alilipua bomu alilokuwa amebeba katika msikiti ndani ya kituo cha polisi huko Peshawar (kaskazini-mashariki), na kuua zaidi ya maafisa 80 wa polisi.

Wachambuzi wanasema wanamgambo katika maeneo ya zamani ya kikabila yanayopakana na Afghanistan wamejizatiti tangu kurejea madarakani kwa Taliban nchini Afghanistan.

Bajaur, ambapo mlipuko huo ulitokea, ni mojawapo ya wilaya saba zilizojitenga zinazopakana na Afghanistan. Eneo hilo limekuwa kitovu cha vita vya kimataifa dhidi ya ugaidi.

Pakistan iliwahi kukumbwa na mashambulizi ya karibu ya kila siku ya mabomu, lakini operesheni kubwa ya kijeshi iliyoanzishwa mwaka 2014 kwa kiasi kikubwa imerejesha utulivu. Usalama umeimarishwa tangu wakati huo, huku Kaskazini Magharibi ikidhibitiwa na mamlaka ya kitaifa ya Pakistani baada ya sheria kupitishwa mnamo 2018.

(Pamoja na mashirika)

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.