Pata taarifa kuu
RWANDA-BURUNDI-WAKIMBIZI

Mamia ya raia wa Burundi wafukuzwa Rwanda

Rwanda iliwafukuza siku za hivi karibuni mamia ya raia wa Burundi waliokua katika ardhi yake. kwa mujibu wa serikali ya Rwanda, raia hao walikuwa hawatimizi masharti ya kuishi Rwanda.

Wakimbizi wa Burundi waliopigwa picha Aprili 10, 2015 Rwanda.
Wakimbizi wa Burundi waliopigwa picha Aprili 10, 2015 Rwanda. © AFP PHOTO / STEPHANIE AGLIETTI
Matangazo ya kibiashara

Uhusiano kati ya Rwanda na Burundi uliotumbukia kwa zaidi ya mwaka mmoja katika mgogoro mkubwa wa kisiasa, unaendelea kudorora kila kukicha. Bujumbura inaituhumu mara kwa mara Kigali kuwasaidia waasi kujaribu kuipindua serikali yake. Wakati ambapo Kigali imekua ikikanusha tuhuma hizo.

Kwa mujibu wa Seraphine Mukantabana, Waziri wa Rwanda mwenye dhamana ya Wakimbizi, zoezi hili la kuwafukuza raia hao lilifanyika kama sehemu ya operesheni ya kawaida kwa raia wa kigeni wanaoishi nchini Rwanda kinyume cha sheria. "Tulikuwa na idadi ya raia wa Burundi waliokua wametawanyika nchini kote na ambao hawakuwa na vibali vinavyowaruhusi kuishi nchini hapa," Waziri Mukantabana amesema. "Tuliwaomba kutafuta vibali au kutafuta hadhi ya ukimbizi lakini walipuuzia. Wale waliokataa kutekeleza masharti hayo walirejeshwa nyumbani kwao, " amendelea kusema, huku akihakikisha kuwa hajui idadi kamili ya watu waliorejeshwa Burundi.

Kwa mujibu wa muungano wa waandishi wa habari wa Burundi (SOS Media Burundi), watu hao wanasadikiwa kufikia idadi ya zaidi ya 800 waliolazimika kuondoka Rwanda tangu Ijumaa wiki iliyopita. Kwa mujibu wa waandishi hawa, baadhi ya raia hao walikua wakiishi nchini Rwanda kwa miaka mingi.

Kama Waziri wa Rwanda mwenye dhamana ya Wakimbizi amehakikisha kwamba operesheni hii "haikuwalenga pekee raia wa Burundi," afisa wa Rwanda, ambaye hakutaka kutajwa jina lake, ameshtumu: tangu kuanza kwa mgogoro maelfu ya Wanyarwanda walikimbia Burundi kufuatia mateso na unyanyasaji walivyotendewa wakati ambapo wale waliokua hawana vibali vya kuishi humo walifukuzwa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.