Pata taarifa kuu
HAKI-SHERIA

Burundi: Waziri Mkuu wa zamani Alain-Guillaume Bunyoni ahukimiwa kifungo cha maisha

Waziri Mkuu wa zamani wa Burundi, Alain-Guillaume Bunyoni, amehukumiwa siku ya Ijumaa na Mahakama ya Juu kifungo cha maisha jela, hasa kwa kutaka kupindua serikali na kutishia maisha ya rais.

Wakati wa kesi hiyo iliyofunguliwa miezi mitatu iliyopita, Jenerali Bunyoni alikana mashtaka yote na kuomba aachiliwe huru, akitaja "ukosefu wa ushahidi" kwa kuunga mkono shtaka hilo.
Wakati wa kesi hiyo iliyofunguliwa miezi mitatu iliyopita, Jenerali Bunyoni alikana mashtaka yote na kuomba aachiliwe huru, akitaja "ukosefu wa ushahidi" kwa kuunga mkono shtaka hilo. AFP - TCHANDROU NITANGA
Matangazo ya kibiashara

Jenerali Bunyoni, ambaye alikua Waziri Mkuu mwezi Juni 2020, alifutwa kazi mnamo mwezi Septemba 2022, siku chache baada ya Rais Evariste Ndayishimiye kushutumu majaribio ya "mapinduzi ya serikali".

“Waziri Mkuu huyo wa zamani anahukumiwa kifungo cha maisha jela kwa makosa saba aliyokuwa akituhumiwa, likiwemo la kupanga njama dhidi ya mkuu wa nchi kupindua utawala wa kikatiba, jaribio la kumuua mkuu wa nchi kwa msaada wa tambiko, kudharau utawala wa kikatiba. Kumtukana Mkuu wa Nchi na Waziri Mkuu au hata kuhatarisha usalama wa ndani wa nchi", kulingana na shirika la habari la AFP kikinukuu chanzo cha mahakama, ambacho hakikutaka kutajwa jina.

Pia alikutwa na hatia ya kujitajirisha kinyume cha sheria na kuyumbisha uchumi. Mahakama imeamuru kutaifishwa kwa nyumba nne na majengo yake, pamoja na kiwanja na magari 14, kwa mujibu wa chanzo hicho.

Mahakama hiyo ilifuata matakwa ya mwendesha mashtaka ambaye aliomba kifungo cha maisha jela wakati wa kesi hiyo iliyokuwa ikisikilizwa mbele ya Mahakama ya Juu ya Burundi iliyoendeshwa katika chumba cha gereza kuu la Gitega (katikati), mji mkuu wa kisiasa wa nchi hiyo, ambapo anazuiliwa. Bw. Bunyoni alikamatwa Aprili 2023 katika mji mkuu wa kiuchumi Bujumbura usiku wa kuamkia maadhimisho ya miaka 51 ya kuzaliwa kwake.

Washitakiwa wenza sita

Alikuwa kwenye kesi pamoja na washtakiwa wenzake sita. Watano kati yao, ikiwa ni pamoja na afisa wa polisi mwenye cheo cha Kanali, Désiré Uwamahoro na afisa mwandamizi katika idara ya ujasusi (SNR) Destino-Samuel Bapfumukeko, wamehukumiwa vifungo vya kuanzia miaka 3 hadi 15 jela, kulingana na chanzo cha mahakama; mwendesha mashtaka wa umma aliomba kifungo cha miaka 30 jela. Mshtakiwa wa sita ambaye ni dereva aliachiliwa huru.

Wakati wa kesi hiyo iliyofunguliwa miezi mitatu iliyopita, Jenerali Bunyoni alikana mashtaka yote na kuomba aachiliwe huru, akitaja "ukosefu wa ushahidi" kwa kuunga mkono shtaka hilo.

Kwa muda mrefu Bwana Bunyoni alikuwa akizingatiwa kuwa ndiye nambari mbili wa kweli wa utawala na kiongozi wa watu mwenye msimamo mkali kati ya majenerali wanaofanya kazi nyuma ya pazia la utawala. Hapo awali alikuwa Waziri wa Usalama wa Umma (2007-2011 kisha 2015-2020).

Evariste Ndayishimiye alichukua wadhifa wa rais wa Burundi mwezi Juni 2020 baada ya kifo cha ghafla cha Pierre Nkurunziza. Ikiwa jumuiya ya kimataifa imekaribisha ufunguzi fulani wa nchi tangu kuwasili kwake madarakani, tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa ilithibitisha mnamo mwezi Septemba 2021 kwamba hali ya haki za binadamu imesalia kuwa "mbaya" nchini Burundi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.