Pata taarifa kuu

Washington: Mpinzani wa Rwanda Paul Rusesabagina amewasili Marekani

Paul Rusesabagina, mkosoaji mkubwa na mpinzai wa Rais wa Rwanda Paul Kagame na shujaa wa filamu ya 'Hotel Rwanda', amewasili Marekani baada ya kuachiliwa siku ya Ijumaa na kupita Qatar, Ikulu ya White House imetangaza hivi punde.

Paul Rusesabagina, wakati huo akizuiliwa Kigali, mji mkuu wa Rwanda. Septemba 25, 2020.
Paul Rusesabagina, wakati huo akizuiliwa Kigali, mji mkuu wa Rwanda. Septemba 25, 2020. AFP Photos/Simon Wohlfahrt
Matangazo ya kibiashara

 

Mwanasiasa huyo amekuwa akiishi uhamishoni Marekani na Ubelgiji tangu mwaka 1996, kabla ya kukamatwa mjini Kigali mwaka 2020 katika mazingira ya kutatanisha, aliposhuka kwenye ndege aliyodhani inaelekea Burundi. Aliachiliwa baada ya zaidi ya siku 900 gerezani.

“Nimefurahi kumkaribisha Paul Rusesabagina Marekani. Tuna furaha kuwa naye tena katika ardhi ya Marekani, na kuunganishwa tena na familia yake na marafiki ambao wamekuwa wakisubiri siku hii kwa muda mrefu,” amesema Jake Sullivan, Mshauri wa Usalama wa Kitaifa wa Marekani.

"Ninashukuru kwa wale ambao tumefanya nao kazi kwa karibu katika serikali ya Rwanda kufanikisha hili," ameongeza.

Baada ya kukaa jela kwa zaidi ya siku 900 bwana Rusesabagina aliachiliwa chini ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali ya Marekani na Rwanda kwa usaidizi wa Qatar ambapo alifika siku ya Jumatatu kabla ya kuondoka kuelekea Marekani.

Kuhukumiwa kwa 'ugaidi'

Aliyekuwa meneja wa hoteli katika mji mkuu wa Rwanda, Bw. Rusesagabina aliokoa maisha ya mamia ya watu wakati wa mauaji ya kimbari dhidi ya ya Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani mwaka 1994. Historia yake ilifanywa kuwa maarufu kwa filamu ya Hotel Rwanda, iliyotolewa mwaka wa 2004. Baadaye akawa mkosoaji na mpinzani mkali wa Rais Paul Kagame, na kuunda chama chake cha kisiasa.

Mazungumzo juu ya kuachiliwa kwake yalianza mwishoni mwa mwaka 2022 na mafanikio yalitokea wiki iliyopita katika mazungumzo kati ya Rais Kagame na Emir wa Qatar, chanzo kinachofahamu suala hilo kimesema. Baada ya kukaa uhamishoni kwa miaka mingi, alikamatwa mjini Kigali mwaka 2020 wakati ndege aliyofikiri ilikuwa ikielekea Burundi ilipotua kwenye uwanja wa ndege wa Kanombe nchini Rwanda.

Mpinzani huyo alihukumiwa kuanzia mwezi Februari hadi Julai 2021 kwa makosa tisa, likiwemo la "ugaidi", kwa mashambulizi yaliyofanywa na FLN, kundi lililotajwa kuwa la kigaidi na Kigali, ambalo liliua watu tisa mnamo mwaka 2018 na 2019.

Paul Rusesabagina alikiri kushiriki katika uanzishwaji wa chama cha Rwandan Movement for Democratic Change (MRCD) mwaka wa 2017, ambapo FLN inachukuliwa kuwa tawi lake la kijeshi, lakini amekuwa akikana kuhusika na mashambulizi hayo.

Katika barua ya mwezi Oktoba 2022 iliyochapishwa Ijumaa na serikali, alihakikishia kwamba atajiepusha na maisha ya kisiasa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.