Pata taarifa kuu

Tanzania: Sherehe za kuwaaga wahanga 19 wa ajali ya ndege zafanyika Bukoba

Mamia ya watu wameaga wahanga 19 wa ajali ya ndege iliyoanguka katika Ziwa Victoria ilipokuwa aikijaribu kutua katika uwanja wa ndege wa mji wa Bukoba, moja ya majanga mabaya zaidi ya anga katika historia ya Tanzania. 

Waokoaji wakijaribu kuokoa abiria kutoka kwa ndege ya Precision Air, iliyoanguka katika Ziwa Victoria huko Bukoba, Tanzania, Novemba 6, 2022.
Waokoaji wakijaribu kuokoa abiria kutoka kwa ndege ya Precision Air, iliyoanguka katika Ziwa Victoria huko Bukoba, Tanzania, Novemba 6, 2022. REUTERS - STRINGER
Matangazo ya kibiashara

Ndege ya Precision Air PW494 kutoka mji mkuu wa kiuchumi Dar es Salaam ilianguka Jumapili asubuhi ikiwa na watu 43 kwenye maji ya ziwa kubwa zaidi barani Afrika, takriban mita 100 kutoka uwanja wa ndege wa jiji hili kaskazini-magharibi mwa nchi. Ajali hiyo ilisababishwa na hali mbaya ya hewa, polisi imesema.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa na mawaziri kadhaa wamehudhuria Jumatatu na mamia ya watu katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kwa ajili ya ibada ya maombi iliyoongozwa na viongozi wa dini ya Kiislamu na Kikristo, kabla ya miili ya wahanga kukabidhiwa kwa familia zao.

Televisheni ya Tanzania ilirusha moja kwa moja hafla hiyo iliyofanyika, huku mvua nyingi ikinyesha.

Shirika la ndege la Precision Air, shirika kubwa la ndege la kibinafsi nchini Tanzania, limesema ndege iliyoanguka ni ATR 42-500, iliyotengenezwa na kampuni ya ATR ya Ufaransa na Italia, na ilikuwa na watu 43 - abiria 39 akiwemo mtoto mchanga na wafanyakazi wanne.

Watu 24 walinusurika kwenye ajali hiyo.

Video zilizorushwa kwenye vyombo vya habari vya ndani zilionyesha ndege hiyo ikiwa imezama kwa kiasi kikubwa katika maji na waokoaji, wakiwemo wavuvi, wakijaribu kuwaokoa walionusurika.

Rais Samia Suluhu Hassan alitoa pole kwa waliofikwa na ajali hiyo. "Nawaombea marehemu wapumzike kwa amani na majeruhi wapone haraka," alisema kwenye Twitter, akipongeza pia "walioshiriki katika uokoaji, wakiwemo wakazi wa Bukoba".

Ukosoaji umeongezeka juu ya ukosefu wa ufanisi wa mamlaka wakati wa uokoaji.

“Tutaboresha (...) hatua za Serikali katika kukabiliana na ajali hizo kwa kushirikiana na sekta binafsi”, amebaini Waziri wa Ulinzi, Innocent Bashungwa, wakati wa hafla hiyo.

Waziri wa Uchukuzi Makame Mbarawa amewataka watu kuwa watulivu wakati uchunguzi unaendelea.

Precision Air, inayomilikiwa na shirika la ndege la Kenya Airways, ilianzishwa mwaka 1993 na inaendesha safari za ndege za ndani na nje ya nchi pamoja na kukodisha ndege za kibinafsi kwa maeneo ya kitalii kama vile Hifadhi ya Kitaifa ya Serengeti na Visiwa vya Zanzibar.

Ajali hii inajiri miaka mitano baada ya vifo vya watu kumi na mmoja katika ajali ya ndege ya kampuni ya Safari kaskazini mwa Tanzania.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.