Pata taarifa kuu
SUDANI KUSINI-USALAMA

Karibu raia 14,000 wakimbia machafuko kaskazini mwa Sudan Kusini

Kwa siku tano, Detoh Rie amekuwa akiishi kwenye mabwawa ya Kaunti ya Leer. Kama watu wapatao 14,000, amekimbia ghasia zilizozuka hivi karibuni katika eneo hili la Sudan Kusini, ambalo limetumbukia katika machafuko kwa takriban muongo mmoja.

Uharibifu uliofanywa na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini.
Uharibifu uliofanywa na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini. AFP PHOTO/WORLD VISION/A.HAMER
Matangazo ya kibiashara

Mapigano yalizuka katika eneo hili la Kaskazini mwa Jimbo la Unity siku ya Ijumaa kati ya wanajeshi wa SPLA-IO wa Makamu wa rais Riek Machar na vikosi vilivyojitenga na kundi hilo mwezi Agosti mwaka uliyopita na kujiunga na kambi ya hasimu wa Machar, Rais Salva Kiir.

Uongozi wa kijeshi wa pande zote mbili zenye makao yake makuu katika mji mkuu Juba mara moja ulitoa wito wa kukomeshwa kwa uhasama.

Mapigano hayo yaliendelea hadi Jumapili, na raia katika kaunti hii yenye historia mbaya - ambapo njaa iliripotiwa mnamo mwaka 2017, wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya umwagaji damu kati ya Kiir na Machar kati ya 2013 na 2018 - wamepoteza mali na wapendwa wao.

"Askari walivamia vijiji vyetu na kuchoma nyumba zetu nyingi. Walichukua ng'ombe wetu, mbuzi wetu na kuua watu," amesema Detoh Rie, aliyehojiwa kwa simu kutoka eneo hili gumu kufikiwa.

"Chakula chetu chote kimeteketezwa majumbani mwetu, hatuna chochote cha kula," baba huyo mwenye umri wa miaka 51 amesema.

Katika taarifa yake siku ya Jumatatu, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (Unmiss) ulisema kwamba "vijiji vingi kusini mwa mji wa Leer (vimeporwa na kuchomwa moto" na pia walionyesha wasiwasi kuhusu ripoti za uharibifu wa bandari jirani ya Adok, kwenye Mto wa White Nile, "mji wa pili wa kiuchumi wa Jimbo".

Walinda amani "wameimarisha doria", msemaji Linda Tom aliliambia shirika la habari la AFP siku ya Jumanne, akitoa "ripoti zinazotia wasiwasi za unyanyasaji wa kingono, uporaji na uharibifu".

Kulingana na Mlinzi wa Kaunti ya Leer Stephen Taker, watu 13,930 waliohamishwa walikuwa wamesajiliwa kufikia Jumatatu. "Kila kitu walichokuwa nacho kiliporwa. Hali ni mbaya sana," aliambia AFP.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, mapigano haya yanazidisha hali ya kibinadamu ambayo tayari ni "mbaya" katika eneo hili la Sudan Kusini, nchi changa zaidi duniani ambayo imekuwa ikiishi katika machafuko ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama tangu uhuru wake kutoka kwa Sudan mwaka 2011.

Jimbo la Unity limeathiriwa kwa miezi kadhaa na mafuriko mabaya zaidi kuwahi kutokea katika miaka 60.

Ngome ya Riek Machar, eneo la Leer hapo awali imekuwa ikiathiriwa mara kwa mara na mapigano kati ya wanajeshi wanaomuunga mkono Kiir na Machar.

Ilikuwa ni moja ya vitovu vya mzozo wa kibinadamu uliosababishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano, ambavyo vilisababisha karibu watu 400,000 kuuawa na mamilioni kuyahama makazi yao. Njaa iliripotiwa katika eneo hili kati ya mwezi Februari na Juni 2017.

Mnamo mwaka wa 2018, Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa alishutumu uwezekano wa uhalifu wa kivita katika eneo hili.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.