Pata taarifa kuu
KOMBE LA DUNIA BRAZIL 2014

Ivory Coast yaanza vema michuano ya kombe la dunia, Uingereza yaumbuka mbele ya Itali

Hatimaye bara la Afrika hapo jana walau lilipata ahueni baada ya wawakiloshi wengine kwenye michuano ya kombe la dunia timu ya taifa ya Ivory Coast kufanikiwa kupata ushindi kwenye mchezo wake wa awali dhidi ya Japan, huku Uingereza ikiangua pua mbele ya Italia. 

Mchezaji wa Ivory Coast, Gervinho akishangilia bao na mwenzake, Didier Drogba.
Mchezaji wa Ivory Coast, Gervinho akishangilia bao na mwenzake, Didier Drogba. REUTERS/Ruben Sprich
Matangazo ya kibiashara

Kwenye mchezo huo wa kundi C ambako kuna timu za Japan, Colombia, Ugiriki na Ivory Coast wenyewe, oinatajwa kuwa miongoni mwa makundi magumu pia kwenye michauno ya mwaka huu nchini Brazili.

Gervinho akiwania mpira na mchezaji wa Japan.
Gervinho akiwania mpira na mchezaji wa Japan. REUTERS/Stefano Rellandini

Ivory Coast ambayo iliingia uwanjani kwa kujiamini huku ikiongozwa na viungo bora kwa sasa duniani kama vile Yaya Toure, Serey Die na Sheikh Tiote waliisumbua vema kiungo ya timu ya taifa ya Japan ambayo ilikuwa ikiongozwa na mchezaji wa Manchester United Shinji Kagawa na Keisuke Honda.

Kwenye mchezo huu ambao Japan waliuanza kwa kasi kwa kufanya mashambulizi ya kushtukiza kwenye lango la Ivory Coast, ni wazi walionesha kuwa walikuja kutafuta ushindi kwenye mechi hiyo ambayo hata hivyo wachambuzi wa mambo wanaona kuwa timu zote mbili zilikuwa na uwezo wa kupata ushindi kutokana na uwiano uliopo wa kimkakati.

mshambuliaji wa Ivory Coast, Didier Drogba.
mshambuliaji wa Ivory Coast, Didier Drogba. REUTERS/Stefano Rellandini

Juhudi za Japan zilizaa matunda kwenye dakika ya 16 ya mchezo ambapo mchezaji Keisuke Honda alifanikiwa kuipatia bao la kuongoza timu yake baada ya kuunganisha pasi nzuri aliyopewa na Nagatomo ambaye aliwazidi ujanja mabeki wa Ivory Coast.

Bao hili lilidumu hadi mapumzimko ambapo Japan ilikuwa ikiongoza kwa bao moja, kipindi cha pili kilianza kwa kasi, ambapo vijana wa Japan kwa mara nyingine waliongeza presha kwenye lango la wawakilishi wa Afrika lakini safari hii juhudi zao hazikufua dafu.

Kiungo wa pembeni na kati wa Japan, Shinji Kagawa akimiliki mpira kiustadi
Kiungo wa pembeni na kati wa Japan, Shinji Kagawa akimiliki mpira kiustadi fifa.com

Katika dakika ya 64 ya mchezo, timu ya Ivory Coast walifanikiwa kusawazisha bao kupitia kwa mchezaji Wilfred Bony ambaye alitumia vizuri mpira wa pasi aliopewa na mchezaji Serge Aurier ambaye nae alitumia uwezo kutoa pasi ya mwisho kwa Bony.

Kipindi cha pili aliingia mchezaji nguli na mkongwe kwenye timu hii, Didier Drogba ambaye alichukua nafasi ya Serey Die.

Katika dakika ya 66 Ivory Coast walifanikiwa kupata bao la pili na la ushindi kupitia kwa mchezaji wake, Gervinho anayekipiga na klabu ya Roma ya Italia, ambaye nae alipokea pasi nzuri mara hii tena kutoka kwa Aurier ambaye alikuwa mwimba kwa timu ya Japan.

Mshambuliaji wa Ivory Coast, Wilfred Bony akifunga bao la kusawazisha dhidi ya Japan kwenye fainali za kombe la dunia 2014
Mshambuliaji wa Ivory Coast, Wilfred Bony akifunga bao la kusawazisha dhidi ya Japan kwenye fainali za kombe la dunia 2014 fifa.com

Ushindi huu sasa unawaweka wawakilishi hawa kwenye nafasi nzuri ya kufanya vema kwenye mchezo ujao, ambapo watacheza siku ya Alhamisi ya Juma linaloanza dhidi ya Colombia ambayo nayo ilipata ushindi kwenye mchezo wake uliopita dhidi ya Ugiriki.

Mchezo mwingine wa kundi C uliwakutanisha timu ya taifa ya Colombia waliokuwa na kibarua dhidi ya timu ya taifa ya Ugiriki, kwenye mchezo ambao hata hivyo ilitoa matokeo mengine ya kushangaza baada ya wagiriki kukubali kichapo cha mabao 3-0 kwenye mchezo ambao dhahiri Colombia walikuwa wameutawala.

Ugiriki ikiongozwa na viungo, Katsouranis, Maniatis, huku kwenye safu ya ushambuliaji wakichagizwa na wachezaji, Gekas na Samaras ambao katika kipindi cha kwanza walijaribu kuonesha nia ya kutaka kupata mabao ya mapema kuwachanganya Colombia.

Hata hivyo ujanja wa Ugiriki ulibainika mapema na Colombia ambao nao waliamua kuziba nafasi kwenye safu ya kiungo ya Ugiriki hali iliyowafanya Ugiriki kushindwa kupeleka mashambulizi yao kwa wakati.

Bao la kwanza la Colombia lilipatikana kwenye dakika ya 5 kupitia kwa Pablo Armero ambaye alitumia pasi nzuri aliyopewa na Cuadrado, dakika ya 58, Colombia walifanikiwa kupata bao la pili lililofungwa na Guiterrez ambaye aliunganisha vema pasi ya Aguilar ambaye aliwazidi ujanja mabeki wa timu pinzani na kutoa pasi ya mwisho kwa mfungaji.

Bao la tatu na la mwisho la Colombia lilipatikana kwenye dakika za nyongeza baada ya mwamuzi kuongeza dakika tatu, ambapo bao hili lilifungwa na James Rodriguez ambaye aliunganisha vizuri pasi aliypoewa na mchezaji, Juan Cuadrado.

Mechi nyingine zilikuwa ni za kundi D ambako kuna timu za Uruguay, Costa Rica, Uingereza na Italia.

Mchezo wa kundi D ambao ulikuwa unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka duniani ambao wanafuatilia fainali za mwaka huu nchini Brazil, ulikuwa ni ule uliowakutanisha miamba ya dunia, timu ya taifa ya Uingereza ambao walikuwa na kibarua dhidi ya timu ya taifa ya Italia “The Azzuris”, kwenye mchezo ambao Italia walichomoza na ushindi mnono wa mabao 2-1.

Kwenye mchezo huo ambao ulionekana wazi kila upande kupania kutaka kuchomoza na ushindi ulishuhudia kila kocha akiwatumia wachezaji muhimu wa timu yake, kwa upande wa Kocha Roy Hodgson alimtumia mshambuliaji wake tegemezi, Wayne Rooney na Daniel Sturridge huku kwa upande wa kocha wa Italia akimtumia kiungo mkongwe Andrea Pirlo huku kwenye safu ya ushambuliaji alimtumia mchezaji mtukutu, Mario Barloteli.

Walikuwa ni Italia ambao walikuwa wa kwanza kuandika bao katika dakika ya 35 ya mchezo kupitia kwa Claudio Marchisio ambaye alitumia vema mpira wa pasi alioupata kutoka kwa Marco Veratti, dakika mbili baadae timu ya taifa ya Uingereza ilifanikiwa kusawazisha bao hilo kupitia kwa Sturridge ambaye alitumia vizuri mpira wa pasi aliopewa na Wayne Rooney.

Wakati mpira huu ukionekana kana kwamba ungemalizika kwa sare, timu ya taifa ya Italia ilifanikiwa kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wake Super Mario Barloteli ambaye aliunganisha mpira uliopigwa na Antonio Candreva, bao ambalo lilimaliza ubishi wa nani kuibuka kidedea kwenye mchezo huo.

Mara baada ya mchezo kocha wa Uingereza, alisema hakatishwi tamaa na matokeo haya hasa baada ya kupoteza mchezo wa kwanza tu, na kwamba anajipanga kwaajili ya mchezo wa pili dhidi ya Uruguay, mchezo utakaofanyika Alhamisi ya juma linaloanza.

Mchezo wa mwisho kwenye kundi D ulizikutanisha timu ya taifa ya Uruguay ambayo ambayo ilikuwa na kibarua dhidi ya timu ya Costa Rica kwenye mchezo ambao katika kile ambacho wengi hawakutarajia, Costa Rica wakachomoza na ushindi mnono wa mabao 3-1.

Timu ya taifa ya Costa Rica
Timu ya taifa ya Costa Rica Reuters

Uruguay ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wake hatari, Edson Cavan ambaye alifunga kwa njia ya tuta, na kuwapa matumaini makubwa mashabiki wa timu hiyo ambayo ilicheza bila ya Luis Suarez.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo Costa Rica waliliandamana lango la Uruguay na kufanikiwa kupata bao kwenye dakika ya 54 ya mchezo kupitia kwa Joel Cambell ambaye alikuwa mwimba mkubwa kwa safu ya ulinzi ya Uruguay ambao walikuwa wakimkaba wawili wawili bila mafanikio.

Cosat Rica walizidisha mashambulizi ambapo katika dakika ya 57 beki Oscar Duarte aliipatia bao la pili timu yake baada ya kuunganisha pasi ya Christian Balanos, bao la tatu na la ushindi kwa Costa Rica lilifungwa katika dakika ya 84 ya mchezo na mshambuliaji Marco Urena akipokea pasi nzuri kutoka kwa Joel Campbell.

Leo usiku kutakuwa na mechi nyingine za kundi E ambapo Uswis watakuwa na kibarua dhidi ya Ecuador, wakati Ufaransa wenyewe watakuwa na kibarua dhidi ya Honduras wakati Argentina watakuwa na kibarua na timu ngeni kwenye michuano ya mwaka huu Bosnia-Herzegovina.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.